Waziri wa Nchi,
Ofisi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa
amesema kuwa miradi ya TACTIC katika
miji 11 inaenda kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Mhe. Mchengerwa
ameyasema leo jijini Dodoma wakati wa utiaji saini mikataba 12 ya utekelezaji
wa miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) kwa miji ya
Morogoro, Songea, Tanga, Korogwe, Babati, Shinyanga, Bukoba, Bariadi, Lindi,
Iringa na Njombe.
Amesema miradi hiyo
pia inaenda kuimarisha huduma za kiuchumi kwa wananchi hususan upande wa mauzo
na manunuzi kwa kuongeza thamani ya biashara nchini ambapo mazingira ufanyaji
wa biashara kwenye ngazi za miji na majiji yanaenda kuboreshwa nchini.
“Tunakusudia
kuhakikisha kwamba utekelezaji wa miradi hii inatekelezwa kwa wakati, hatuna
changamoto ya fedha kwahiyo sitegemei kuona mkandarasi ana legalega.”
“Baadhi ya
wakandarasi wakilipwa fedha wanapeleka kwenye miradi mingine, hili sitokubali
hata kidogo,” alisisitiza.
Aidha, Waziri
Mchengerwa ameonya tabia ya kuchepusha fedha za miradi kunakofanywa na baadhi
ya wakandarasi, akiapa kutengua mikataba ya wakandarasi wa namna hiyo katika
utekelezaji wa miradi ya TACTIC inayotekelezwa kwenye Miji 45 ya Tanzania bara.
Miradi ya TACTIC
iliyosainiwa leo ni ya Miji 11 ya Tanzania Bara, ikiwa ni muendelezo wa
utekelezaji wa miradi ya TACTIC kwenye miji 45 ambayo imekuwa ikinufaika na
ujenzi wa barabara za viwango vya lami, taa za barabarani, mifereji ya maji ya
mvua, ujenzi wa vituo vya mabasi na daladala,
ujenzi wa masoko ya bidhaa na mazao mbalimbali, bustani za mapumziko
pamoja na vivuko vya maji, miradi yote hii ikihusisha takribani Dola za
Marekani Milioni 410, bila ya kodi ya Ongezeko la thamani VAT, ikiwa ni Mkopo
wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.



0 Maoni