Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezipongeza Kampuni za Total
Ernergies na Super Star Fowarders – SSF
kwa kuweza kufikia viwango vya juu vya usalama vya usafirishaji huku
akiwataka wasafirishaji wengine kufuata
nyayo zao kwa kuwa kampuni hizo ni mfano mzuri wa kuigwa.
Dkt. Biteko amesema
hayo Juni 25, 2025 jijini Dar es salaam wakati akishiriki katika maadhimisho ya
miaka 30 ya ushirikiano kati ya Kampuni ya Super Star Fowarders (SSF) na Total
Energies.
“Leo tumekusanyika hapa kusherehekea hafla ya
miaka 30 ya ushirikiano baina ya Kampuni zetu hizi mbili za Total Ernergies na
Super Star Fowarders. Katika kipindi hicho chote, mmekuwa washirika wakubwa wa
kimataifa katika usafirishaji wa bidhaa mbalimbali hususan kwa kutumia matenki
maalum, hakika, binafsi nimefarijika sana
na hongereni sana,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kupitia
ushirikiano huo umewezesha upatikanaji
wa uhakika wa mafuta nchini na kutoa ajira kwa mamia ya vijana pamoja na kuvutia nchi za jirani kutumia Bandari ya Dar
Es Salaam kupitishia mizigo yao na kutoa fursa kwa Watanzania.
Ametoa wito kwa
wasafirishaji wote wa mizigo kwa kutumia malori nchini wazingatie viwango vya juu vya
usalama barabarani kwa kuhakikisha malori yao yanawekwa vifaa vyote vya usalama kama vile
GPS kufuata miongozoi liyopo.
Fauka ya hayo, Dkt.
Biteko amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na
wafanyabiashara wote na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kazi ikiwa ni pamoja
na kuweka sera zenye kutabirika ambazo zitawalinda na kuvutia wawekezaji zaidi
nchini.
Waziri wa Uchukuzi,
Prof. Makame Mbarawa amewataka wasafirishaji kuzingatia usalama barabarani kwa
kuwa suala hilo sio sera tu bali ni kwa maslahi mapana ya Taifa na ajali za barabarani zinasababisha hasara
kubwa ikiwemo uhai wa watu na uchumi wa nchi. Aidha, ametoa wito kwa
wasafirishaji nchini kutumia barabara zilizopo kwa kuzingatia viwango.
Balozi wa Ufaransa
nchini, Mhe. Anne Sophie amesema siku hiyo ni muhimu kwa Tanzania na Ufaransa
kwa kuadhimisha miaka 30 ya ushirikiano kati ya kampuni hizo mbili ambao
umekuwa na faida akitolea mfano mafunzo kwa madereva na matumizi ya vifaa na mifumo ya kuzingatia usalama
barabarani.
Naye, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Super Star
Fowarders (SFF), Bw. Seif A. Seif
amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake na jitihada
zinazosaidia kuimarisha na kukuza sekta ya usafirishaji nchini.
Kwa upande wake,
Makamu wa Rais Mwandamizi wa Kampuni ya
Total Energies Kanda ya Afrika – Huduma za Masoko, Bw. Jean Phillipe Torres
ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na
dhamira yake katika kuimarisha sekta ya nishati nchini.




0 Maoni