Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa, uchaguzi wa wanafunzi wa
kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi
zilizopo, hivyo hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule
kutokana na ukosefu wa nafasi za kufanya mabadiliko hayo.
Waziri Mchengerwa
amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu uchaguzi
wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi kwa
mwaka 2025.
Waziri Mchengerwa
amesema jumla ya wanafunzi 214,141 wakiwemo wasichana 97,517 na wavulana
116,624 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi
ikijumuisha wanafunzi 1,028 wenye mahitaji maalum.
“Muhula wa kwanza kwa
wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza tarehe 08 Julai, 2025, waliopangwa
wanapaswa kuanza kuripoti shuleni kuanzia tarehe 06 Julai, 2025 na siku ya
mwisho ya kuripoti ni tarehe 21 Julai, 2025, na waliopangwa kwenye Vyuo vya
Elimu ya Ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika vyuo
walivyopangiwa,” Mhe. MChengerwa amesisitiza.
Akizungumzia ubora wa
ufaulu kwa kuangalia madaraja, Mhe. Mchengerwa ameainisha kuwa, watahiniwa
223,372 (41.23%) walipata ufaulu wa Daraja la I – III, hali inayoonesha kuwa
ufaulu wa watahiniwa wa mwaka 2024 umeongezeka kwa asilimia 5.36%
ikilinganishwa na ufaulu wa Daraja la I – III wa watahiniwa 198,394 (35.87%) wa
mwaka 2023.
Aidha, Waziri
Mchengerwa amewapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha
Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi na kuwahimiza kuendelea kufanya bidii katika
kujifunza ili waweze kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya Elimu ya Juu baada ya
kuhitimu Kidato cha Sita na Vyuo vya Elimu ya Ufundi.
Sanjari na hilo, Mhe.
Mchengerwa amewapongeza walimu, wazazi na walezi wote kwa juhudi walizozifanya
katika malezi na ufundishaji hali iliyowezesha wanafunzi kufaulu vizuri, na
amewataka kuendelea kuwa na moyo wa kusimamia na kufuatilia maendeleo ya watoto
shuleni.
Uchaguzi wa Wanafunzi
wa Kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule za Sekondari na Vyuo vya Elimu ya
Ufundi vya Serikali umefanyika kwa kuzingatia utekelezaji wa Sera ya Elimu na
Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na Mtaala ulioboreshwa, hivyo wanafunzi waliochaguliwa
ni kutoka Shule za Serikali, zisizo za Serikali na watahiniwa wa kujitegemea
waliofanya mtihani chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.
Na. James K.
Mwanamyoto OR-TAMISEMI


0 Maoni