Waziri wa Fedha, Mhe.
Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na
Norway umefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii
ikiwemo miradi ya elimu, usambazaji wa umeme vijijini yenye thamani zaidi ya sh.
bilioni 188.
Dkt. Nchemba
alibainisha hayo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Norway nchini, Mhe. Teni Tone Tennis, ambapo pamoja na mambo mengine,
walijadiliana namna ya kukuza maeneo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kilimo, mabadiliko
ya tabianchi, kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF,
na ukusanyaji wa mapato ya ndani ya nchi.
“Norway imekuwa
mshirika wetu wa karibu katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya kiuchumi
nchini ikiwemo kuwezesha usambazaji wa umeme mkoani Lindi kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini wenye thamani ya bilioni 48.1,” alisema Mhe. Nchemba.
Alisema kuwa Serikali
ya Norway pia imetoa ufadhili wa kujiendeleza kielimu kwa wahandisi wanawake
kwa kiasi cha sh. bilioni 4.68 ikiwa ni juhudi za kuleta usawa wa kijinsia
nchini.
Dkt. Nchemba
aliongeza kuwa mradi mwingine unaofadhiliwa na Norway ni Programu ya Usalama wa
Jamii ya Kukuza Uzalishaji (PSSN II), tangu mwaka 2020 ambapo nchi hiyo
imechangia kiasi cha shilingi bilioni 136.5.
‘’Baada ya mafanikio
ya Mpango wa PSSN II unaotarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2025, Serikali ya
Tanzania inaandaa PSSN III ambao utazingatia kuisaidia jamii katika mazingira
ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kiuchumi, hivyo tunatamani Serikali
ya Norway itaendelea kuunga mkono utekelezaji wa programu hii kwa manufaa ya
wananchi wetu,” alisema Dkt. Nchwemba.
Aliongeza kuwa tangu
miaka ya 1990, Serikali ya Norway imekuwa ikiisaidia Tanzania kupitia Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Kisasa wa Kodi
uliomalizika mwaka 2022 ambapo sasa, Serikali inasubiri ripoti rasmi ya Kikosi
Kazi cha Rais kuhusu mageuzi ya kodi, kabla ya kuanza kutekeleza mapendekezo
yake.
Aidha, Dk. Nchemba
alisisitiza kuwa Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Norway
katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Tatu wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26), hususan kwenye sekta za nishati,
elimu, ukuaji wa uchumi, na mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa
Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan, imejizatiti kuendeleza ushirikiano wa karibu na Serikali ya Norway kwa
ajili ya ustawi wa wananchi wa nchi hizo mbili.
Kwa upande wake
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Teni Tone Tennis, alisema kuwa nchi yake
itaendeleza kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha kuwa nchi inafikia
maendeleo ya kiuchumi na kijamii huku akipongeza hatua ya maendeleo iliyofikiwa
na kuhimiza kuendeleza juhudi hizo katika ujenzi wa Tanzania mpya, yenye
maendeleo jumuishi na endelevu.
Alipongeza mafanikio
ya Serikali katika utekelezaji wa mradi wa treni ya mwendokasi (SGR) ambao ni
nguzo muhimu ya kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na kuunganisha nchi za ukanda
wa Maziwa Makuu kiuchumi na kijamii na kuwa ni mfano wa kuigwa kwani
umerahisisha shughuli za kiuchumi.
‘‘Ninapenda kutoa
pongezi za dhati kwa hatua ya kuanza kusafirisha mizigo kupitia reli ya SGR, ni
hatua muhimu si tu kwa Tanzania, bali kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Kupitia hatua hii, Tanzania inaonesha uongozi wa mfano ambao mataifa ya jirani
yanaweza kujifunza na kuiga’’, alisema Mhe. Tennis.
Alisema Tanzania
inazidi kutambulika kimataifa kwa juhudi zake katika sekta ya usafiri na
miundombinu ambapo mbali na maendeleo ya reli, imebarikiwa kuwa na rasilimali
nyingi zenye thamani kubwa zikiwemo gesi asilia, ardhi yenye rutuba kwa kilimo,
pamoja na madini ya kila aina.
Ushirikiano wa
Tanzania na Norway umejikita katika nyanja za kiuchumi na kijamii hatua ambayo
Norway imeahidi kuuendeleza kupitia uwekezaji wa mitaji na kukuza biashara kwa
manufaa ya nchi hizo mbili.
Na. Saidina Msangi -WF,
Dodoma
0 Maoni