Kamishna wa Uhifadhi
TANAPA, Musa Nassoro Kuji jamefanya kikao kikazi na
Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Kitulo iliyopo mkoani, Njombe.
Katika kikao kazi
hicho kilichofanyika jana Kamishna Kuji amewataka Maafisa na Askari kujipanga vilivyo katika
kufanya kazi hasa katika msimu huu mpya wa utalii ambao unakwenda kuanza mwezi
Julai 2025 ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kikamilifu.
“Ni fahari kubwa
kwetu TANAPA kushiriki kuchangia katika ujenzi wa Taifa letu kupitia uratibu na
usimamizi wa shughuli za utalii katika hifadhi za Taifa na maeneo ya Malikale
yaliyokasimiwa kwa TANAPA. Mafanikio hayo ni matunda ya kila mmoja wetu katika
kuhifadhi maliasili hizi tulizokabidhiwa kuzitunza kwa niaba ya Watanzania. Mpaka
siku ya jana (juzi) 23.06.2025 Shirika limeweza kukusanya shilingi billioni 480 ikiwa
imesalia shilingi 20 kufikisha nusu trillioni” alisema Kamishna Kuji.
“Bodi ya Wadhamini ya
Shirika imenituma niwahakikishie ushirikiano wa kutosha “full support” katika kufanikisha
utendaji kazi wa viwango vya Kimataifa. Tunapoanza mwezi wa saba TANAPA
tunategemea kususanya trilioni ili tuondoke kwenye ukusanyaji wa mabilioni,
hiyo ndiyo kazi iliyo mbele yetu. Hili linawezekana kwa kila mmoja wetu kuchapa
kazi usiku na mchana ili kufikia malengo ya Shirika na Taifa kwa ujumla,”
aliongeza Kamishna Kuji.
Awali, akimkaribisha
Kamishna wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Kitulo, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kusini, Godwell Meng’ataki
alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha Uhifadhi na
Utalii hususani kwa hifadhi zilizopo kusini kwani hifadhi hizo zimekuwa
zikipokea idadi kubwa ya watalii.
“Baada ya Mhe. Rais
wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Samia Suluhu Hassan kucheza Filamu maarufu ya
Tanzania: The Royal Tour” na ile ya “Amazing Tanzania” Hifadhi za Taifa
zilizopo Kusini tumeanza kuona matunda yake kwa kuongeza idadi ya watalii
lakini pia kwa namna ambavyo Bodi ya Wadhamini ya TANAPA imekuwa ikitoa
miongozo kwa Menejimenti ya Shirika ili kutoa huduma zenye viwango vya
Kimataifa kwa watalii. Jitihada hizo zimekuwa chachu ya kuvutia watalii wengi
katika maeneo yetu” alisema Kamishna Meng’ataki.
Kwa upande wake,
Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kitulo Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza, Ally
Hemedi Kimwanga alieleza kuwa “Katika mwaka fedha ujao wa 2025/2026,
unaotarajiwa kuanza mwezi wa Julai 2025 Hifadhi ya Taifa Kitulo imejipanga
vilivyo katika kuhifadhi na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi
hiyo pamoja na mapato yatokanayo na shughuli za utalii. Maafisa na Askari
Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Kitulo tunakuahidi Afande Kamishna kuchapa kazi
yenye viwango vya Kimataifa”.
Pia, Kamishna wa
Uhifadhi Musa Nassoro Kuji leo amefanya ziara ya kikazi na kufanya kikao na
Maafisa na Askari Uhifadhi wa Kanda ya Kusini ya TANAPA iliyopo Rujewa wilayani
Mbarali, Mkoani Mbeya.
Hifadhi ya Taifa
Kitulo ni hifadhi yenye kivutio kikubwa cha uwepo wa maua mazuri yanayovutia na
kupelekea hifadhi hiyo kupewa jina maarufu kama “Bustani ya Mungu”. Pia,
hifadhi hiyo ni miongoni mwa vyanzo vya maji ya Ziwa Nyasa na Mto Ruaha Mkuu
ambapo maji hayo ni muhimu sana kwenye kuchechemua shughuli za uchumi wa nchi
ikiwemo uzalishaji wa umeme, shughuli za kilimo pamoja na uvuvi.
Na. Edmund
Salaho/Kitulo
0 Maoni