Mganga Mkuu wa
Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Dkt.Diocles Ngaiza amesema zaidi ya wagonjwa
700 watapatiwa matibabu ya macho katika kambi ya matibabu ya wagonjwa wenye
Mtoto wa jicho kwa siku Saba yanayoendelea katika Halmashauri hiyo.
Dkt. Ngaiza ameyasema
hayo wakati alipotembelea kambi hiyo itakayohudumu kwa siku saba ikiwa
imeandaliawa na Taasisi ya Hellen Keller kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais –
TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya mahususi kwa ajili ya kufanya upasuaji wa
Mtoto wa jicho na matibabu mengine ya macho.
“Katika kambi hii
tunatarajia kuhudumia watu zaidi ya 700 hadi sasa kwa siku hizi mbili tu, kuna
wagonjwa zaidi ya 200 wamepatiwa huduma na wako safi kabisa tofauti na
walivyokuja” alisema Dkt. Ngaiza.
Amesema Halmashauri
pia imeiweka mikakati mbalimbali katika kupambana na changamoto hiyo ya macho
ikiwa ni pamoja na kuongeza wataalamu wa macho na kununua vifaa tiba katika
vitengo vya macho katika maeneo ya kutolea huduma za afya.
Aidha, amewataka
wananchi mbalimbali wenye changamoto za macho kujitokeza kwa wingi katika
huduma hiyo ili kuweza kutatuliwa changamoto hizo.
Na. OR - TAMISEMI
0 Maoni