Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya Sh. Trilioni 7.53 katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ufanisi wa asilimia 101.32 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 7.43.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda imeeleza
kuwa ufanisi wa makusanyo ya Robo ya Tatu ya mwaka 2024/2025 ni sawa na ukuaji
wa asilimia 13.47 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Trilioni 6.63
zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2023/24.
Taarifa hiyo
inaeleza kuwa makusanyo yaliyokusanywa katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha
2024/25 yanapelekea TRA kuweza kuweka rekodi ya kipekee katika utekelezaji wa
majukumu yake kwa kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi 9 mfululizo
katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Taarifa ya
Bw. Mwenda inafafanua kuwa katika kipindi cha mwezi Julai – Machi, mwaka wa
fedha 2024/25, TRA imekusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 24.05 sawa na ufanisi
wa asilimia 103.62% ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 23.21, na ukuaji wa
asilimia 17.01 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Trilioni 20.55.
Aidha,
makusanyo hayo ni ya kiwango cha juu kabisa kufikiwa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania kwa kipindi kama hicho toka kuanzishwa kwake, na ni sawa na ongezeko
la asilimia 77 toka kiasi cha Shilingi Trioni 13.59 zilizokusanywa katika
kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2020/21, miaka minne toka Mhe. Dkt. Samia
suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aingie madarakani.
Ufanisi huu
katika makusanyo uliofikiwa mwezi Julai – Machi mwaka wa fedha 2024/25 ni
matokeo chanya ya kutekeleza kwa vitendo maagizo na maelekezo ya Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yanayohusiana na
uongezaji wa uhiari wa ulipaji kodi kupitia uboreshaji wa huduma kwa walipakodi
na uboreshwaji wa shughuli za biashara nchini.
Bw. Mwenda
katika taarifa yake amewashukuru Walipakodi kwa kuendelea kulipa Kodi kwa hiari
na kuiamini TRA.
0 Maoni