Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza walimu na uongozi
wa Shule ya Al Muntazir kwa kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa
upendo mkubwa.
Dkt. Biteko
ametoa pongezi hizo jana Aprili 6, 2025 katika viwanja vya Shule ya Al Muntazir
iliyopo jijini Dar es salaam mara baada ya kufanya matembezi ya Maadhimisho ya
Siku ya Usonji Duniani iliyofanyika shuleni hapo kitaifa.
Amesema mara
baada ya Mungu kumuumba mwanadamu mtu mwingine anayeweza kumuumba mwanadamu kwa
kumfundisha na kumkuuza kimaarifa na maadili ni mwalimu.
“ Tumeona
watoto hawa wanafanya kazi mbalimbali, wanafundishwa na wanaongozwa vizuri niwapongeze walimu wote wa shule hii
mnaofundisha watoto wenye mahitaji maalum pamoja na uongozi wa shule mmefanya
kazi hii kwa watoto kwa ujuzi mlionao mmefanya wanaweza kuimba kuandika,
kutengeneza sabuni na vitu mbalimbali,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea “
Tumekusanyika hapa ili kuadhimisha Siku ya Usonji Duniani. Pia kuuambia ulimwengu kuwa
tunatambua na kujali kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu. Shule za Al
muntazir zimeanza na sisi washiriki tuna wajibu wa kuendeleza na kuienzi azma
hii.”
Aidha,
uongozi wa shule za Al muntazir ulianzisha shule ya watoto wenye mahitaji
maalumu Januari, 2013 na kutoa malezi kwa watoto wenye ugumu katika kujifunza
kati ya umri wa miaka 4 hadi 20. Ambapo sasa ina wanafunzi 100 kutoka wanafunzi
39 walikuwepo mwaka 2013.
Vilevile,
Dkt. Biteko amesema uongozi wa hiyo unafanya jitihada mbalimbali ili
kuhakikisha kuwa huduma ya namna hiyo inawafikia wadau wengine wa nje.
Ametaja
baadhi ya jitihada kuwa ni kuendeleza
raslimali watu na nyingine ili kukabiliana na changamoto zilizopo pamoja na
kutoa huduma ya mafunzo kwa walimu wa kawaida na wale wa watoto maalum katika
maeneo mengine ya Dar es salaam, Arusha na Zanzibar.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema “ Hii ni zaidi
ya shule ni tiba kwa vile ndani ya kufundisha wanatibu pia kwa kutumia fursa
mbalimbali.”
Akizungumza
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar wa salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe.
Edward Mpogolo amewashukuru walimu wa Shule hiyo kwa kuwatunza watoto hao wenye
mahitaji maalum ambao wameendelea kuwasaidia kwa kubuni miradi mbalimbali
ikiwemo ufugaji wa sungura.
Naye, Rais wa
Jumuiya ya Khoja Shia Itha Ashar Jamaat,
Mohammed Raza Dewji amesema kuwa
wanatarajia kujenga kituo cha kisasa kitakachohudumia wanafunzi 500 ambacho
kitajumuisha huduma mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi na kusaidia
kuongeza ushirikiano wa wanafunzi karibu na jamii ili kuwajengea uwezo wa
kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali katika maisha yao siku za baadae.
“Hii si ndoto bali ni ushirikiano wa kila
mmoja katika jamii kwa kujitoa na kuchangia kwa moyo kwa sababu watoto hawa
wanahitaji huduma zaidi,” amesema Dweji.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni