Katibu Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa
msingi wa sera za CCM utabakia kuwa ni maendeleo ya watu pamoja na amani na utulivu
wa nchi.
Balozi
Nchimbi aliyasema hayo jana Jumapili, tarehe 6 Aprili 2025, alipokuwa
akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Songea katika maeneo ya Liziboni,
Uwanja wa Majimaji na Mshangano, ambapo wananchi walikusanyika kwa hamasa kubwa
kumsikiliza licha ya kuwa kwenye ziara nyingine za kikazi.
Katika eneo
la Liziboni, Balozi Nchimbi alilazimika kusimamisha msafara wake ili kuzungumza
na wananchi waliomsimamisha njiani akitokea Nyasa. Alitumia fursa hiyo
kuwashukuru wananchi wa Songea kwa mchango wao mkubwa uliomuwezesha kufahamika
kitaifa na kimataifa.
Katika Uwanja
wa Majimaji, alihutubia umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakimsubiri wakati
alipofika kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ghorofa lenye fremu 50 za
CCM Mkoa wa Ruvuma. Katika hotuba yake, aliwaomba wananchi wa Songea, mkoa
mzima na nchi nzima kwa ujumla kujiandaa kushiriki kwa wingi Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.
Akiwa
Mshangano, ambako alizindua rasmi fremu 50 za tawi la CCM la eneo hilo, Balozi
Nchimbi alisisitiza tena umuhimu wa ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi
mkuu, akieleza kuwa ni kwa njia hiyo ndipo maendeleo na ustawi wa taifa
yanaweza kufikiwa kwa kasi na kwa manufaa ya wote.
Kwa ujumla,
ziara ya Katibu Mkuu huyo ilionesha mapokezi makubwa ya wananchi na kiu ya
kusikia mwelekeo wa chama chao kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
0 Maoni