Mwenyekiti wa
Bodi ya Wadhamini - TANAPA Jen. Mst. George Waitara akiongozana na Wajumbe
wenzake wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania lililopewa
dhamana ya kusimamia hifadhi 21 za Taifa alisema kuwa Hifadhi ya Taifa Ruaha
kuwa kitovu cha utalii Kusini mwa Tanzania kutokana na ubora wa miundombinu ya
kisasa ya utalii iliyowekezwa kupitia Mradi wa REGROW unaofadhiliwa na Benki ya
Dunia.
Aliyasema hayo jana Aprili 06, 2025 wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi sita inayotekelezwa
katika hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa Tanzania ikiwa na ukubwa wa kilometa za
mraba 19,822 huku ikibeba mikoa ya Dodoma, Iringa huku eneo kubwa la hifadhi
hiyo likiwa katika wilaya za Mbarali na Chunya zilizopo mkoani Mbeya.
Alisema,
“Tumetembelea miradi sita (6), mitano imekamilika isipokuwa jengo la abiria la
uwanja wa ndege Kiganga ambao ujenzi wake unaendelea, kwa hakika nimefurahishwa
na usimamizi wa menejimenti ya Ruaha kwa kuwa bega kwa bega na wakandarasi hao,
kwa hifadhi ambazo bado miradi hii inasuasua itabidi tuwatume kwenu. Kwani
ninyi mmekuwa mfano mzuri wa kuigwa na hifadhi nyingine.”
Hata hivyo,
Waitara aliwataka Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kuhakikisha
inawasimamia Wakandarasi ili kukamilisha jengo la Abiria lililofikia asilimia
92, likamilike ili lianze kutumika kwa ndege zitakazoshusha abiria (watalii)
katika uwanja huo wenye uwezo wa kupokea ndege za uwezo wa kubeba abiria 50 kwa
wakati mmoja.
Waitara
aliongeza, “Kwa miradi mitano iliyokamilika ambayo ni Nyumba za kulala wageni
(Cottages), Hostel, Kituo cha Ikolojia, Majengo kwa ajili ya malazi ya madereva
na waongoza wageni pamoja na Kituo cha kutolea taarifa za uhifadhi na utalii
ziwekewe thamani ili zianze kutumika, kwa kufanya hivyo tutavutia watalii wengi
kutembelea hifadhi hii.”
Naye CPA.
Hadija Ramadhani Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini - TANAPA na Mwenyekiti wa Kamati
ya Ukaguzi na Utawala Bora alisema, “Kwa
hakika Hifadhi ya Taifa Ruaha mmeitendea haki fedha ya REGROW, majengo yote
yamependeza na ni mfano wa kuigwa kwa hakika kazi zingefanyika hivi kama taifa
tungefika mbali hivyo niwahimize kuweka thamani ili majengo hayo yatumike kwani
majengo yakikaa muda bila kutumika huharibika.”
Sambamba na
ukamilishaji wa majengo hayo na miundombinu mingine ndani ya hifadhi hiyo inayotegemewa kuwa kitovu kikubwa cha
utalii upande wa kusini mwa Tanzania, Wajumbe hao wa bodi walitaka kujua
usimamizi wa masuala mbalimbali ya jengo hilo la Abiria.
Akitoa ufafanuzi
wa jinsi ya usimamizi wa jengo hilo Naibu Kamishna wa Uhifadhi na
Maendeleo ya Biashara Massana Mwishawa
alisema, “TANAPA tumejipanga kuhakikisha usalama, usafi na huduma mbalimbali
zinatolewa na wataalamu wetu wa ndani kwani baadhi ya Maafisa na Askari
wameshapewa mafunzo na wengine wataendelea kupewa mafunzo kuendana na mahitaji
ya wakati huo.”
Naye,
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kusini - Godwell Meing’ataki
alisema kuwa kukamilika kwa majengo hayo mapya yatayohudumia watalii na watu
mbalimbali kumeongeza uhitaji wa watumishi, hivyo shirika wakati sasa shirika
kuona namna bora ya kuongeza watumishi kwa ajili ya kutoa huduma bora kulingana
na viwango vya kimataifa.
Kabla ya
kuanza kwa ziara hiyo, Wajumbe hao wa Bodi pia walipata wasaa wa kusikiliza
wasilisho kutoka kwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Abel Mtui Mkuu wa Hifadhi ya
Taifa Ruaha kuhusu shughuli mbalimbali za Uhifadhi na utalii zinazotekelezwa
huku matumizi ya teknolojia yakichukua nafasi kubwa katika uhifadhi na ukusanyaji
wa maduhuli.
Hifadhi ya
Taifa Ruaha imeendelea kuwa hazina kubwa nchini Tanzania kutokana na umuhimu wa
kuhifadhi wanyama na ndege mbalimbali adimu na waliopo hatarini kutoweka pamoja
na mto “The Great Ruaha”kama chanzo cha nishati katika mabwawa ya Mtera, Kidatu
na Bwawa la Kimkakati la Mwl. Nyerere, maji kwa matumizi ya majumbani na uvuvi
uliohalalishwa hususani bwawa la Mtera kwa ajili ya wananchi kujipatia kipato,
hivyo kukauka kwake hakuiathiri hifadhi tu bali ni watanzania wengi wanaotegemea
mto huu.
Na. Jacob
Kasiri - Ruaha
0 Maoni