Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejizatiti kukabiliana na changamoto ya
wanyama wakali na waharibifu kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo matumizi ya
teknolojia za kisasa ili kulinda uhai wa wananchi na mali zao.
Haya
yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb)
alipokuwa akikagua uzio wa umeme wenye urefu wa kilomita zipatazo 33 unaotumika
kutatua changamoto ya wanyama wakali na waharibifu kwa kutenganisha Pori la
Akiba Ikorongo na vijiji vipatavyo 06 katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Mhe.
Kitandula amefanya ziara hiyo kwa lengo la kukagua ufanisi wa uzio huo na
kujionea manufaa yanayopatikana kwa wananchi wa vijijini vinavyopakana na uzio
huo.
Katika ziara
hiyo Mhe. Kitandula hakusita kuwataka wahifadhi kuendelea kubuni njia nyingine
zenye tija za kutatua changamoto ya wanyama wakali na waharibufu kwa kuwa
serikali ina wajibu mkubwa wa kulinda uhai wa wananchi na mali zao, sambamba na
kuendeleza Uhifadhi wa Maliasili hizi tulizopewa na Mwenyezi Mungu kama zawadi.
“ Taifa
limetukabidhi Wizara ya Maliasili na Utalii jukumu kubwa na zito la kulinda
maliasili zinazohusisha wanyama, malikale na misitu kwaniaba ya Watanzania.
Sambamba na jukumu hilo tunao wajibu vilevile kwaniaba ya serikali kuhakikisha
uhai na mali za wananchi wanaozunguka maeneo ya Hifadhi vinalindwa. Hivyo
lazima tutumie maarifa kupata majawabu ya changamoto inayolisumbua Taifa
kwasasa ya wanyama wakali na waharibifu na wakati huo huo maliasili nazo
zilindwe ili ziendelee kuchangia katika uchumi wa nchi yetu,” alisema Mhe.
Kitandula.
Mhe.
Kitandula aliongeza kuwa Serikali ipo tayari kuingiza maeneo mengine nchini
yenye changamoto ya wanyama wakali na waharibifu kwenye matumizi ya teknolojia
ya uzio wa umeme, hatahivyo alisema
matumizi hayo lazima yaongozwe na ushauri wa kisayansi, hivyo amewataka
wahifadhi wafanye tafiti na kuja na ushauri wa kisayansi utakaowezesha
kuanzishwa matumizi ya ya uzio wa umeme katika maeneo mengine nchini.
Aidha,
alihimiza wahifadhi kuendeleza matumizi mchanganyiko ya mbinu mbalimbali za
kisasa katika kusaidia kulinda maliasili za wanyamapori na kuondoa changamoto
ya migongano ya wanyama wakali na waharibifu. Alihimiza kuongezeka kwa matumizi
ya ndege nyuki, mabomu baridi, uvishaji wa mikanda ya mawasiliano, uvunaji wa
wanyama wakorofi, na matumizi ya kamera kwenye uzio wa umeme ili kuuongezea
ufanisi.
Uzio wa umeme
katika Pori la Akiba Ikorongo ulijengwa mwaka 2019 na Kampuni ya Grumeti
Reserves (T) Ltd kwa idhini ya Wizara ya Maliasi na Utalii. Uzio huo wenye
urefu wa Kilometa 33 umejengwa ndani ya
mpaka wa Pori la Akiba Ikorongo bila kugusa maeneo ya vijiji. Mpaka huo unapita
katika vijiji sita (06) vinavyopakana na pori hilo ambavyo ni Mbilikili,
Bonchugu, Rwamchanga, Kazi, Miseke na Park Nyigoti katika
Wilaya ya Serengeti.
Na. Anangisye
Mwateba-Fort Ikoma - Serengeti
0 Maoni