Taasisi ya
Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi imepongezwa kwa kazi kubwa inayoifanya ya
kuandaa na kutoa askari wengi wanaofanya kazi kubwa kwenye maeneo
yaliyohifadhiwa nchini yanayohusisha Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Maeneo
ya Hifadhi za Wanyamapori za Jamii, na Misitu hivyo kufanya nchi kuwa na
Uhifadhi endelevu ambao ni uti wa mgongo wa Sekta ya Utalii nchini.
Pongezi hizi
zimetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb)
alipokuwa akifunga mahafali ya 60 fungu la kwanza kwa udahili wa mwezi Machi
katika mwaka wa masomo 2024/2025 ya wahitimu wa mafunzo ya Uaskari wa Uhifadhi
wa Wanyamapori na Himasheria katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi
jijini Mwanza.
Akizungumzia
changamoto ya Ajira, Mhe. Kitandula amewataka wahitimu kutumia fursa ya uwepo
wa Kampuni ya Ulinzi ya Taasisi ya
Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi (PASCO) kuomba kujiunga nayo na kuweza
kupangiwa vituo pale huduma inapohitajika kutoka kwa wadau mbalimbali wa
uhifadhi. Aidha, amewataka wahitimu
watakaopata nafasi za ajira PASCO kutumia fursa hiyo kujiongezea uzoefu na
maarifa, na kutangaza jina la Taasisi kwa kuwa mabalozi wazuri.
Vilevile Mhe.
Kitandula alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau mbalimbali wanaojishughulisha
na shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na biashara ya utalii zikiwemo taasisi
za serikali na sekta binafsi kuwaajiri na kuendelea kuwatumia vijana hawa ili
kuongeza tija na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
Katika hatua
Nyingine Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori
Pasiansi Prof. Agnes Sirima ameahidi kuwa watajikita katika kuhakikisha taasisi
ya taaluma ya wanyamapori Pasiansi inatoa mafunzo bora katika sekta ya uhifadhi
wa maliasili na uongozaji watalii.
Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi mwaka huu imefikisha miaka 59 toka kuanzishwa kwake mwaka 1966 kwasasa ipo katika maandalizi ya maadhimisho ya miaka 60 toka kuanzishwa.
Na. Anangisye
Mwateba - Pasiansi Mwanza
0 Maoni