Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewataka Watanzania kutegemea kupata umeme wa uhakika baada ya Mradi wa
kufua umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere uliokuwa ukisubiriwa kwa shauku
kubwa na Watanzania kukamilika rasmi.
Dkt. Biteko ameyasema hayo April 5, 2025 baada ya kutembelea
Mradi huo akiwa ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na
uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira, Mhe. Hamadi Masauni pamoja na Viongozi wengine
mbalimbali.
Amesema hivi sasa mitambo yote tisa imekamilika na inafanya
kazi tayari, amefafanua kuwa kukamilika kwa Mradi huo kumechangiwa na maono ya
Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliupokea Mradi
ukiwa katika asilimia 33 ya utekelezaji wake na ndani ya kipindi cha miaka
minne ya Uongozi wake ameweza kuukamilisha Mradi.
‘’Tumekuja leo tukiwa na furaha kubwa kwamba mitambo yote
tisa imekamilika inazalisha umeme na nina furahi kuwajulisha Watanzania kuwa
ile ndoto ya kuwa na umeme kutoka kwenye chanzo hiki kikubwa barani Afrika
imekamilika, kazi iliyobaki ni kuimarisha miundombinu ya kuwafikishia
watanzania umeme,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amesema kutokana na nchi kuwa na uwezo wa
kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa sasa Serikali iko katika mchakato wa
kukamilisha mazungumzo na nchi ya Zambia kwa ajili ya kuwauzia umeme na
tayari njia ya umeme ya kuunganisha nchi hizo mbili inajengwa.
‘’Kile ambacho tumekua tukikiongea miaka mingi kwamba
Tanzania itakuwa na uwezo wa kuuza umeme nje ya nchi sasa imetimia katika
kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya sita baada ya msukumo mkubwa wa Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan tuna mshukuru sana Mheshimiwa Rais.’’
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na
Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo amesema kukamilika kwa Mradi huu ni
ukombozi wa kiuchumi huku Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira, Mhe. Hamadi Masaun amesema Tanzania imeingia katika historia barani
Afrika ambapo amesema kazi kubwa iliyobaki ni kutunza vyanzo vya maji ili
kuulinda Mradi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biiteko amelipongeza Shirika la umeme Tanzania TANESCO
kwa usimamizi mzuri katika kutekeleza mradi huu kwa kiwango cha kimataifa na
kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mha. Gissima Nyamo-Hanga kwa
jitihada zake katika kusimamia miradi mbalimbali ya umeme nchini.
Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere umegharimu zaidi ya
Shilingi Trilioni 6.5 ambapo mpaka sasa serikali imeshalipa zaidi ya
asilimia 99.5.
0 Maoni