WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Tanzania ni Taifa
lililopata mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali za maendeleo katika
kipindi cha miaka 61 ya Muungano.
Amesema hayo leo (Ijumaa, Aprili 25, 2025) wakati
akizungumza na maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Getrude Mongela.
Mheshimiwa Majaliwa amefanya ziara ya siku moja katika
Wilaya ya Ukerewe ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano.
Amesema kuwa Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar
umewezesha kujenga Taifa imara na lisiloyumba “Muungano huu umewezesha kuwa
na Taifa ambalo limepata mafanikio
katika miradi mbalimbali ya maendeleo Bara na Visiwani, Muungano huu ni tunu
ambayo kila mmoja anapaswa kuilinda, kuienzi na kuisemea popote.”
“Kwenu hapa Ukerewe Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa
na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mabilioni mengi ya fedha yameletwa
kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta elimu, afya, maji,
mawasiliano na maeneo mengine muhimu. Serikali hii imefanya mabadiliko mengi.”
Kadhalika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya
ujenzi wa mradi wa hospitali ya rufaa ya kibingwa yenye hadhi ya mkoa
inayojengwa katika Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza.
Akizungumza baada ya kukagua hospitali hiyo Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa hospitali hiyo itawawezesha wakazi wa Wilaya hiyo
kutotembea umbali mrefu ikiwemo kwenda
Mwanza kufuata huduma za kibingwa za afya.
Hospitali hiyo inajengwa na Mkandarasi M/S Dimetoclasa
Realhope Limited JV Mponela Construction & Co. Ltd kwa gharama ya shilingi
bilioni 25.03 na inategemewa kukamilika ifikapo Julai 8, 2026.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa
jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza ambalo
ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 3.7.
Akizungumzia kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa
amewataka Watanzania kuendelea kuwa na imani na Serikali na amewahakikishia
kuwa miradi ya maji itatekelezwa kutokana na umuhimu mkubwa wa huduma hiyo kwa
jamii.
Akizungumza kuhusu maboresho ya vivuko katika Wilaya ya
Ukerewe Meneja Vivuko Kanda ya Ziwa , Vitalis Bilauri amesema Serikali
inakamilisha ujenzi wa vivuko vitano ambavyo vitatoa huduma katika Wilaya ya
Ukerewe na visiwa vyake.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma Anselim
Namala amesema kuwa Meli ya MV Clarius ipo katika hatua ya ukaguzi ili
ukarabati uanze kufanyika.
Pia, ameongeza kuwa ukarabati wa meli ya Mv Butiama
umekamilka na sasa upo katika hatua ya mwisho ya ukaguzi na kupata vibali kabla
ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi hivi karibuni.
Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Ujenzi wa Hospitali Teule ya Rufaa ya Kibingwa yenye hadhi ya Mkoa Wilayani Ukerewe ni hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya katika Wilaya ya Ukelewe na Visiwa Vyake.
"Hospitali hii itakapo kamilika itakuwa ni miongoni mwa hospitali zenye hadhi kubwa za utoaji huduma nchini, Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya makubwa katika sekta ya Afya na Ujenzi wa Hospitali hii ni uthibitisho wa mafanikio hayo."
0 Maoni