Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema wananchi wa wilayani Arumeru, mkoani Arusha na Watanzania kwa
ujumla wana kila sababu ya kumshukuru na kumuombea Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 25, 2025 katika mkutano
wa hadhara uliofanyika Tengeru Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha ambapo amesema
katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia wilaya ya Arumeru
imepokea zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
“Arusha DC imepata fedha kiasi cha shilingi bilioni 49.6 na
Wilaya ya Arumeru imepokea zaidi ya shilingi
bilioni 51 kwa ajili ya shughuli
na miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Akiwa Wilayani humo amekagua mradi wa kuboresha miundombinu
ya Hospitali ya wilaya Arumeru na mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la Chuo
cha Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo ameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa
miradi hiyo.
Ametoa mfano wa
miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kuwa ni miradi ya umeme na Tanzania ni kati
ya nchi chache barani Afrika ambazo zimefanikiwa kuzalisha umeme kwa asilimia
100.
Miradi mingine iliyotekelezwa ni ujenzi wa shule, maabara,
hospitali, vituo vya afya, miradi ya kilimo pamoja na barabara.
Licha ya mafanikio hayo Dkt. Biteko ameeleza kuwa Serikali
ni sikivu na itaendelea kutatua changamoto za barabara, maji na madaraja
zilizopo mkoani Arusha pamoja na maeneo mengine nchini.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewahimiza Watanzania kudumisha
amani na mshikamano kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo yaliyopatikana.
“ Tusijaribu
kuichezea amani, amani inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Rais Samia ameapa
kuilinda amani hii kwa gharama yeyote. Nitumie nafasi hii kumkumbusha kila
Mtanzania kuwa tunu ya amani ndiyo inayofanya tuendelee kuwa salama na bila
amani hatuwezi kuwa na chochote,” amesisitiza
Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano,
Watanzania waendelee kudumisha amani, umoja na kuwa na mshikamano usioangalia
dini, kabila wala itikadi za siasa. Aidha, Muungano ulipo wa Tanganyika na
Zanzibar ni wa kipekee na wenye faida
nyingi, huku akitaja kauli mbiu yake kuwa
“Muungano wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa; Shiriki Uchaguzi
Mkuu wa Mwaka 2025.”
Vilevile, amewahimiza wananchi kushiriki katika Uchanguzi
Mkuu na kumchagua Rais, wabunge na madiwani mwezi Oktoba mwaka huu.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema kuwa
katika mchoro wa mkoa uliopo kutakuwa na barabara ya itakayojengwa eneo la Usa River pamoja na
arabara kuelekea Uwanja wa Ndege Kisongo ili kupunguza adha ya usafiri kwa
wakazi wa Arusha.
Ameendelea kusema kuwa barabara ni ajenda kubwa katika Mkoa
huo na kuwapongeza wananchi kwa kuelewa
kuwa maendeleo ni mchakato na kuwa madiwani na wabunge wamekubaliana kipaumbele
chao kwa mwaka 2025/26 ni barabara.
Ametoa pongezi kufuatia miradi ya umeme mkoani humo
“Tunakushukuru Naibu Waziri Mkuu kwa kutuletea mradi wa umeme wa REA na
wananchi wanaunganishiwa umeme kwa shilingi 27,000. Mradi utakaokamilisha umeme katika vijiji na
vitongoji vyote kupata umeme katika mkoa wa wetu,”
Awali akizungumza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amesema kuwa Taasisi
ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ni taasisi ya kipekee inayotoa huduma za
maendeleo ya jamii nchini ambayo ilianzishwa mwaka 1963.
Ameeendelea kusema kuwa Taasisi hiyo ni tegemeo la kuzalisha
wataalamu wa maendeleo ya jamii na inaendelea na ujenzi wa jengo la utawala litakalo
gharimu shilingi bilioni 5.6 na hadi sasa wametumia shilingi bilioni 2.7.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa kutupatia
fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu ambao ukikamilika utatatua changamoto ya
uhaba wa ofisi kwa kuwa na ofisi 44 zitakazo hudumia watu 94,” amesema Dkt.
Jingu.
Aidha, Dkt. Biteko ameendelea na ziara yake siku tano mkoani humo ambapo tayari ametembelea Wilaya za Monduli, Longido na Aumeru ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.




0 Maoni