Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki limekutana
na kufanya mkutano wake wa 47 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha
Aprili 25, 2025.
Mkutano huo umefanyika katika ngazi ya Mawaziri kufuatia
kukamilika kwa Mkutano ya Ngazi ya Wataalamu na Ngazi ya Makatibu Wakuu
iliyofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 24 Aprili 2025.
Mkutano huo umejadili taarifa za utekelezaji wa masuala
mbalimbali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yakiwemo mapendekezo ya Mpango wa
Bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Aidha, Mkutano huo umepokea Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za
Jumuiya iliyowasilishwa na Kamisheni ya Ukaguzi ya wa Hesabu za EAC inayoundwa
na Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali kutoka Nchi Wanachama wa
EAC kwa mujibu wa Ibara ya 134 ya Mkataba unaoanzisha EAC.
Mkutano huo pia umeendelea kusisitiza Nchi Wanachama
kutekeleza wajibu wa kutoa Michango ya Uanachama, na pia kusisitiza taasisi
zilizo chini ya EAC kutekeleza majukumu kwa mujibu wa kiwango na ukomo cha
Bajeti iliyopangwa kwa mwaka husika wa Fedha.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mawaziri, Wanasheria Wakuu,
Makatibu Wakuu na Timu za Wataalamu kutoka mamlaka mbalimbali za Serikali za
Nchi Wanachama wa EAC.
Katika Mkutano huo Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Mhe. Dennis Lazaro Londo (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, viongozi wengine na wawakilishi kutoka Tanzania walioshiriki katika Mkutano huo ni pamoja na Mhe. Omar Said Shaban, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Zanzibat, Bw. Onorious J Njole; Mwandishi Mkuu wa Sheria (Akimuwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Dkt. Franklin J Rwezimula; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria akimuwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria), na Upande wa Makatibu Wakuu uliongozwa na Balozi Stephen P. Mbundi; Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
0 Maoni