WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa, amemuagiza Waziri wa Afya, Jenista Mhagama na watendaji wa
Wizara hiyo kukutana na kufanya mapitio ya vigezo ili kukipandisha hadhi kituo
cha Afya cha Mama Ngoma kilichopo kata ya Kwakoa Wilaya ya Mwanga Mkoani
kilimanjaro kuwa hospitali.
Amesema
mwekezaji huyo amefanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Shilingi Bilioni tano kwa
kujenga majengo yenye hadhi na kuweka vifaa vya kisasa hivyo ni lazima Serikali
imuunge mkono kwa kukipandisha kituo hicho.
"Maliza
hatua iliyobaki ipewe hadhi ya hospitali kama kuna eneo mnadhani linatakiwa
kufanyiwa marekebisho mshirikiane nae, kazi anayofanya huyu ni kubwa ya kuiunga
mkono Serikali ya kuwahudumia Watanzania tunamuachaje?". Alihoji.
Ametoa
maelekezo hayo (jana Jumanne Machi 25, 2023) alipokuwa akizungumza na wananchi
baada ya kuzindua Kituo Cha Afya cha Mama Ngoma kilichopo kata ya Kwakoa
Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa
Majaliwa amemshukuru Muwekezaji wa kituo hicho Profesa Ngoma na kumuahidi kuwa
Serikali itaendelea kumuunga mkono.
"Umeniambia
unataka uanzishe chuo cha uuguzi hapa, endelea na taratibu, ongeza ubunifu na
ongeza huduma, Serikali tutakuunga mkono".
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amekagua jengo la utawala la Halmashauri ya
Wilaya ya Mwanga ambalo hadi kukamilika kwake litatumia shilingi bilioni 3.7
ambapo amewaagiza viongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanakamilisha mradi
huo kwa wakati.
Kadhalika,
amewataka madiwani na viongozi wa Halmashauri na Wilaya zote nchini kuhakikisha
wanasimamia ukamilishaji wa miradi yote ambayo iko katika hatua ya
ukamilishaji. “Msisitizo wangu miradi yote ambayo bado haijakamilika ikamilike
kabla ya mwezi wa nane.”
Mheshimwa
Majaliwa amehitimisha ziara yake ya siku moja kwa kuzungumza na wananchi katika
Mkutano wa hadhara uliofanyika Usangi Wilayani Mwanga ambapo amewasihi wananchi
kuendelea kuwa na imani na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Rais
wetu ana nia ya dhati ya kuwatumikia
watanzania na ana mpango kazi mzuri wa kukamilisha miradi ya maendeleo sambamba
na kusogeza huduma karibu na wananchi."
0 Maoni