Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeitaka TANAPA kuendelea kuboresha maeneo ya vivutio vya utalii ili kuvutia idadi kubwa ya wageni na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa.
Hayo
yamezungumzwa jana, Machi 25, 2025, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine
Holle (Mb), wakati wa ziara ya Kamati hiyo iliyolenga kukagua miradi ya
maendeleo pamoja na shughuli zinazotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha.
“Hifadhi hii
ina vivutio vingi vya asili na tumeshuhudia maporomo ya maji pamoja na wanyama
wa aina mbalimbali wakiwa katika maeneo yao ya asili hivyo ni jukumu letu
kuhakikisha kuwa maeneo haya yanaboreshwa zaidi na kufikika kwa urahisi na
wageni wote.”
Aidha, Holle
aliongeza, “Tunahitaji pia kutoa fursa nyingi za uwekezaji kwa watu binafsi
hususani wazawa ili kuongeza ubora wa huduma jambo litakalovutia wageni wengi
kuitembelea hifadhi hii.”
Vilevile,
Holle alisema kuwa kama Kamati wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya
maendeleo inayoendelea ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha ikiwemo ukarabati wa
barabara na ujenzi wa nyumba za kisasa za kulala wageni, hatua hizi ni ishara
ya maendeleo makubwa ambayo yatarahisisha kufikika kwa maeneo mengi na kuimarisha huduma ya malazi kwa wageni.
Akimwakilisha
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Dkt.Robert Fumagwa ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, alitoa
shukrani kwa Kamati hiyo kufika na
kutembelea Hifadhi ya Taifa Arusha kwa lengo la kukagua pamoja na
kuangalia shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.
Dkt. Fumagwa
alisema “Ushauri wa Wajumbe wa Kamati umepokelewa na tutahakikisha mapendekezo
hayo yanafanyiwa kazi na miradi hii inakamilika kwa wakati ili kuongeza ufanisi
wa hifadhi na kuifanya kuwa kivutio bora
kwa watalii wa ndani na nje ya Tanzania.”
Kwa upande
wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru - Amir Mohammed Mkalipa, alitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta miradi
mbalimbali ya maendeleo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha, miradi ambayo
imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Arumeru, huku ikichochea
maendeleo pamoja na kuboresha maisha yao.
Naye, Naibu
Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga, ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini,
alisema kuwa TANAPA itaendelea kuisimamia miradi yote inayojengwa ndani ya
Hifadhi ya Taifa Arusha na kuhakikisha inakidhi viwango vilivyokusudiwa sanjari
na kushirikiana na vijiji vinavyozunguka hifadhi ili kuhakikisha wananchi
wananufaika na uwepo wa hifadhi hiyo.
Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imefanya ziara ya kukagua
miradi miwili ya maendeleo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha. Miradi hiyo ni
pamoja na ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilomita 16, ambayo imegharimu
kiasi cha shilingi milioni 419, pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa za kulala
wageni ambazo gharama yake ni shilingi milioni 204.
Na. Happiness
Sam - Arusha


0 Maoni