Mawakala takribani 120 kutoka nchini Marekani wamefurahishwa
na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini Tanzania ikiwemo utajiri wa
utamaduni mzuri, wanyamapori na mandhari inayovutia.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Excellent Guide Tours and Safaris, Bw. Justin Alfred usiku wa Novemba 7, 2025
katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na
Utalii kwa mawakala hao waliowasili nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio
mbalimbali vya utalii.
“Tuna furaha sote tumeweza kutalii kwa kuona wanyamapori kama tembo, twiga,
simba,nyati na wengine na nipende kuiambia dunia kuwa Tanzania ni nchi salama
na ina watu wakarimu hivyo wasisite kuja kuitembelea,” amesema Bw. Alfred.
Amefafanua kuwa lengo la ziara hiyo ya mawakala nchini
Tanzania ni kuhakikisha dunia yote inafahamu kuhusu Bara la Afrika hasa nchi ya
Tanzania kutokana na utajiri wake na vivutio ilivyonavyo.
Naye, Wakala wa Utalii kutoka kampuni ya Nexion Travel ya
Marekani, Patricia Walker alisema yalikuwa ni matamanio yake tangu akiwa na
umri wa miaka mitano kuitembelea Tanzania hasa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
hivyo amefurahishwa na ukarimu na huduma zilizotolewa tangu awasili nchini na
kwamba amepata kumbukumbu isiyosahaulika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi amewashukuru mawakala hao wa utalii kwa kuitembelea Tanzania na kuwahimiza kuwa mabalozi wazuri wa utalii wanaporudi nchini kwao.



0 Maoni