Tabora Zoo yaendelea kupokea makundi mbalimbali ya watalii

 

Ikiwa zimesalia siku chache kuelekea kufunga mwaka wa 2025, Bustani ya Wanyamapori Hai Tabora, maarufu Tabora Zoo, Hifadhi inayotajwa kubeba historia iliyopea Kwa vipeo inaendelea kuwa kivutio cha makundi mbalimbali ya watalii wanaofika kwa ajili ya shughuli za utalii, mafunzo na kubarizi.

Mnamo Novemba 8, 2025, Umoja wa Akina Mama Mahiri (MMN) kutoka Wilaya ya Sikonge ulifanya ziara maalum katika bustani hiyo ili kujionea vivutio vya kipekee vya utalii vinavyopatikana ndani yake ikiwemo mandhari ya asili pamoja na wanyamapori hai kama tembo, nyumbu, hasa "nyumbu mwongozo wa watalii", ngiri maarufu “Kasongo”, simba, chui na duma, sambamba na spishi mbalimbali za ndege nyuni wakiwemo tausi na kasuku mapenzi, wanaopamba anga la Mkoa wa Tabora  kwa sauti na rangi zao za kuvutia.

Kwa kipindi cha hivi karibuni, Tabora Zoo imejipatia umaarufu mkubwa na kuwa kimbilio la watalii wengi kutoka ndani na nje ya mkoa huo. Hii ni kutokana na ongezeko la wanyamapori hai pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya utalii uliofanywa na Serikali kupitia TAWA, ikiwemo eneo la michezo ya watoto linaloongeza burudani na furaha kwa familia na wageni wanaotembelea bustani hiyo.

Aidha, TAWA inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea hifadhi hiyo, ikiwemo taasisi za serikali, taasisi binafsi, vikundi vya vikoba, vyama na mashirika mbalimbali, kwa ajili ya vikao, mafunzo, sherehe za harusi na shughuli nyingine za kijamii zinazoambatana na utalii.



Chapisha Maoni

0 Maoni