Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepata mafanikio ya kuimarisha
upitikaji wa miundombinu ya barabara za wilaya wenye urefu wa kilometa
144,429.77 kwa asilimia 55 ambapo lengo ni kufikia asilimia 60 ifikapo mwezi
Juni, 2025.
Mafanikio
haya yanatokana na ongezeko kubwa la bajeti ya Wakala kutoka shilingi bilioni
275 hadi shilingi bilioni 870.3 sawa na ongezeko la asilimia 216 kuanzia mwaka
wa fedha 2021/2022 hadi 2024/25.
Hayo
yameelezwa leo tarehe 26/03/2025 Jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Wakala
ya Barabara za Vijijini na Mijini, Mhandisi Victor Seff, katika semina
iliyoandaliwa na TARURA kwa ajili ya Wahariri wa Vyombo vya Habari.
“Mtandao wa
barabara za lami katika kipindi hicho umeongezeka kutoka Km. 2,025.69 hadi Km.
3,337.66, na changarawe kutoka Km.
27,809.26 hadi Km. 42,059.17 na barabara za udongo zimepungua kutoka Km.
112,317.20 hadi Km. 99,032.93. Madaraja yaliyojengwa yamefikia 3,195 na
makalavati 75,620,” amesema Mhandisi Seff.
Aidha,
amesema katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Wakala tunaendelea kufanya
majaribio kwa kutumia teknolojia
mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya mawe 'cobble stone roads' na madaraja
ya mawe 'stone arch bridges' pamoja na teknolojia nyingine katika kuboresha
barabara tunazozisimamia.
Ameeleza kuwa
matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi
ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara, huongeza ufanisi, huokoa
muda, hutunza mazingira kwa gharama nafuu.
“Matumizi ya
teknolojia mbadala na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi kwaajili ya
ujenzi wa barabara na madaraja imeweza kupunguza gharama zaidi ya 50% ambapo
TARURA imeweka kipaumbele cha kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi
ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi,” amesema Mhandisi Seff.
Hata hivyo
Wakala unaendelea na matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara zinazopatikana
maeneo ya kazi na utafiti wa teknolojia mbadala za ECOROADS, Ecozyme, na
GeoPolymer kwenye ujenzi wa barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama,
kupunguza muda wa utekelezaji na kulinda mazingira, amesema Mhandisi Seff.
Amesema jumla
ya madaraja ya mawe 350 yamejengwa ambapo gharama zimepungua kwa kiasi cha
Shilingi bilioni 10. Kwa upande wa majaribio ya teknolojia mbadala Km. 7.95
zimekamilika na Km. 53.76 zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na
ufuatiliaji wa ubora wa teknolojia hizo unaendelea.
“Haya yote ni
matokeo ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mtandao wa
barabara za wilaya, kwa kuwa maeneo ya kilimo vijijini yakiwa yanafikika kwa
mwaka mzima, inaongeza ukuaji wa kilimo na kupunguza umaskini,” amesema
Mhandisi Seff.
0 Maoni