Timu ya wataalamu 53 kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) itajifungia kwa wiki mbili, kuanzia leo Jumatatu, kufanya uchambuzi wa mipango na bajeti za taasisi na mashirika ya umma, kazi ambayo ni muhimu katika kuhakikisha usimamizi mzuri wa rasilimali za serikali.
Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Mashirika
yasiyo ya kibiashara, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Joseph Mwaisemba, alisema
jana kuwa uchambuzi wa bajeti za mwaka wa fedha 2025/26 unahusisha taasisi za umma
252.
“Zoezi la uchambuzi linalofanyika katika Shule
ya Uongozi Mwalimu Nyerere, ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kwamba fedha za
umma zinatumika kwa njia bora na yenye ufanisi,” alisema Mwaisemba.
Ili kufanikisha lengo lililokusudiwa na kwa
kuzingatia matakwa ya kifungu cha 10(2) (c) cha Sheria ya Msajili wa Hazina
SURA 370 na kifungu cha 17(a) cha Sheria ya Bajeti SURA 439, OMH inatakiwa
kufanya uchambuzi wa mipango na bajeti ya Taasisi na Mashirika ya umma
yaliyochini yake.
Lengo lake ni kuidhinisha mikakati, mipango ya
mwaka ya Taasisi na Mashirika ya umma na kuijumuisha katika Mpango wa Taifa wa
Maendeleo kwa ajili ya usimamizi wa utekelezaji na kugharamiwa.
“Utekelezaji wa maelekezo ya Mwongozo huu kwa
ukamilifu utachangia: udhibiti wa matumizi ya fedha za umma na kuleta tija
iliyokusudiwa,” alisema Bw. Mwaisemba, ambaye pia ni msimamimizi wa zoezi la
uchambuzi wa bajeti.
Aidha, alisema utekelezaji utapelekea kuongezeka
kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara na kutoa
fursa sawa za ajira kwa wote.
Sanjari na hilo, alisema utekelezaji wa
maelekezo ya muongozo utapelekea kuendelea kuimarika kwa utoshelevu wa
chakula nchini na kuongeza upatikanaji wa huduma za jamii kwa wote.
Pia, matokeo
tarajiwa (faida kwa Serikali, OMH na mashirika husika) ni pamoja na:
Kuongeza rejesho la uwekezaji wa mashirika ya umma kwa Serikali kupitia
makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, ulipaji wa kodi, utoaji wa huduma, na ajira.
Uwekezaji wa serikali katika taasisi, mashirika
ya umma na wakala za serikali 252 ni Sh83.4 trilioni, ambao ni uthibitisho wa
dhamira ya serikali katika kuimarisha sekta mbalimbali za uchumi na kuhakikisha
kwamba huduma muhimu zinapatikana kwa wananchi.
Sambamba na kuongeza rejesho la uwekezaji wa
serikali, inatarajiwa kushuhudiwa kuimarika kwa utawala bora, kuongezeka kwa
ufanisi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, pamoja na kuelekeza rasilimali
katika maeneo yenye tija ambayo yatachangia katika ukuaji wa uchumi.
Serikali inatoa Mwongozo wa Mpango na Bajeti
ambao unaandaliwa kwa mujibu wa Kifungu Na. 21 cha Sheria ya Bajeti, Sura 439.
Mwongozo huo unalenga katika utekelezaji wa Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025 (TDV 2025) pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, na utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa
ajili ya Uchaguzi ya Mwaka 2020.
Maeneo yanayopewa kipaumbele ni pamoja na
maelekezo kuhusu ulazima wa kuzingatia vipaumbele vya mpango; maelekezo ya
ujumla kuhusu uandaaji wa Mpango na Bajeti; na maelekezo mahususi kwa mashirika
na taasisi za umma.
Vigezo vinavyotumika katika uchambuzi wa mipango
na bajeti ni pamoja na: i. Utekelezaji wa maelekezo mahususi ya Serikali
yaliyotolewa katika mwongozo wa mpango na bajeti wa Serikali katika mwaka
husika. ii. Vigezo vya kupima utendaji wa taasisi na mashirika ya umma ambayo
vinahusu masuala ya kifedha, rasilimali watu, utawala bora, huduma kwa wateja,
na utekelezaji wa majukumu ya msingi ya taasisi.
Matokeo tarajiwa (faida kwa Serikali, OMH na
mashirika husika) ni pamoja na: Kuongeza rejesho la uwekezaji wa
mashirika ya umma kwa Serikali kupitia makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi,
ulipaji wa kodi, utoaji wa huduma, na ajira.
Pia inatarajiwa kushuhudiwa kuimarika kwa
utawala bora, kuongezeka kwa ufanisi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,
pamoja na Kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye tija ambayo yatachangia
katika ukuaji wa uchumi.
Bw. Mwaisemba alitoa wito wa kuwepo kwa
ushirikiano wa karibu kutoka kwa wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi, Menejimenti,
na watumishi wa taasisi na mashirika ya umma.
"Tunahitaji tushirikiane kwa pamoja
kuhakikisha malengo ya serikali ya uanzishwaji wa mashirika hayo yanafikiwa ili
yaweze kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu," alisema.
Hii ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambapo
dhamira ya serikali ni kuondokana au kupunguza utegemezi wa wadau wa maendeleo
katika kutekeleza majukumu yake.
Na. Mwandishi wa OMH
0 Maoni