Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta ya nishati imepiga
hatua kubwa nchini sambamba na kuzalisha umeme wa ziada dhidi ya mahitaji ya
Watanzania.
Dkt. Biteko amesema hayo Machi 23, 2025 jijini Arusha wakati
akitoa takwimu kuhusu ongezeko la
mahitaji ya umeme nchini katika Kikao
cha Baraza Kuu la Wazazi Taifa.
“ Rais Samia amefanya kazi kubwa katika sekta ya nishati
nchini na hivi karibuni, tulikuwa nchini Barbados kueleza mafanikio yetu katika sekta hii kwa kuwa Rais
Samia amefanya jitihada kubwa sana katika ya nishati,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Ili uchumi wa nchi yoyote duniani upatikane
lazima kuwe na sekta ya nishati. Aidha, katika sekta ya nishati ili viwanda
viweze kuendelea umeme unaohitajika ni asilimia 40 na katika sekta ya madini umeme
unaohitajika ni asilimia 30.”
Dkt. Biteko amesema mwaka 2017 hadi 2018 mahitaji ya juu ya
umeme nchini yalikuwa megawati 1045, mwaka 2018 hadi 2019 mahitaji ya juu ya
umeme yalikuwa megawati 1,116 mwaka 2021 hadi 2022 megawati 1,340.7.
“ Mwaka 2022 hadi 2023 mahitaji ya juu yaliyoongezeka na
kufikia megawati 1,470 na mwaka 2024
hadi kufikia sasa mwaka 2025 ni megawati 1,908 ikiwa ni sawa na megawati 262,
ongezeko la mahitaji ya namna hii haliwezi kutokea kama hakuna uwekezaji katika
sekta ya nishati,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Mashine ya tisa ya mtambo wa
kuzalisha umeme katika Bwawa la Julius Nyerere Machi 22, 2025 imekabidhiwa na
kuunganishwa kwenye Grid ya Taifa. Amesisitiza kuwa kutokana na ongezeko hilo
la megawati za umeme Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere pekee linaweza
kutosheleza mahitaji ya nchi licha ya kumalizika kwa muda uzalishaji wa umeme
kwa kutumia mitambo ya Songas.
“Katika kipindi cha
miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan sekta ya nishati imefanya kazi kubwa, Rais Samia ametenda maajabu katika
sekta hii na ameweza kuvutia wawekezaji wengi sana kuja kuwekeza nchini,”
amesema Dkt. Biteko.
Aidha, amesema kuwa Jumuiya ya Wazazi nchini ina wajibu wa
malezi na mazingira na kuwa nishati safi ni eneo mojawapo hivyo Wizara ya
Nishati ina wajibu wa kushirikiana na
wadau mbalimbali ikiwemo Jumuiya hiyo, sambamba na kushirikiana nayo katika
kampeni zake za kupeleka ujumbe kwa jamii.
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amewaasa Watanzania kuzingatia
matumizi bora ya umeme kwa kuacha mazoea yanayosababisha upotevu wa umeme
ikiwemo kuwashaa taa bila kuwa na matumizi nazo.
Ametolea mfano kuhusu matumizi mabaya ya umeme kupitia
utafiti uliofanywa na Wakala wa Nishati wa Kimataifa (International Energy
Agency) ambapo asilimia 30 ya umeme unapotea kutokana na mazoea.
Katika hatua nyingine, taasisi mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) zimewasilisha mada
mbalimbali katika semina hiyo.
Pia, Wizara ya Nishati kupitia taasisi zake za TPDC, REA na
TANESCO zimetoa semina kwa wajumbe wa kikao hicho kuhusu Mkakati wa Taifa wa Matumizi
ya Nishati Safi ya Kupikia 2024 hadi 2034, Matumizi Sahihi ya Nishati Safi ya
Umeme.
Ambapo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Ngeleja Mugejwa ameeleza faida mbalimbali za matumizi ya nishati safi ya kupikia hususan kwa watoto wa kike ambapo kupitia matumizi ya nishati hiyo itawasaidia kupata muda mwingi wa kujisomea kuliko kuandaa na kupika chakula.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni