Uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini utapanda hadi kufikia Megawati 4,031.71 ndani ya mwezi Machi 2025 baada ya kukamilika kwa mtambo wa mwisho wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).
Hayo yameelezwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi
Felschemi Mramba, ambaye amesema kwamba kukamilika kwa mtambo huu kutafanya
mitambo yote tisa (9) ya JNHPP kuwa tayari kwa uzalishaji umeme.
Amesema mbali na jitihada zilizofanywa kwenye uzalishaji umeme, Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya usafirishaji umeme ili kuhakikisha; umeme unafika kwa wateja ukiwa katika viwango bora (quality of power supply) na upotevu wa umeme unapungua.
Pia, kuhakikisha mfumo wa Gridi unaimarika zaidi (improved
system stability) na kupunguza hitilafu mbalimbali za kutoka kwa sehemu au
mfumo mzima na kiwango kikubwa cha umeme kinasafirishwa kutoka kwenye vyanzo
vya uzalishaji kwenda kwa wateja waliopo pembezoni na sehemu mbalimbali za
Mikoa na Wilaya.
Mhandisi Mramba amesema katika jitihada za kupunguza upotevu
wa umeme, kuimarisha mifumo ya umeme pamoja na kuweza kutumia vyanzo vya umeme
vyenye gharama nafuu, Nchi za Tanzania, Kenya na Zambia ziliingia makubaliano
ya kujenga njia ya kusafirisha umeme (Interconnectors) inayounganisha mifumo ya
Gridi ya umeme ya nchi hizo ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa kutumia
umeme wa gharama nafuu unaoweza kupatikana nchi jirani na kupunguza matumizi ya
vyanzo vya gharama kubwa.
Ameeleza kwamba mradi huu ulijulikana kama ZTK
(Zambia–Tanzania–Kenya) ambao mpaka sasa umekamilika kati ya Tanzania na Kenya,
na unaendelea kutekelezwa kati ya Tanzania na Zambia.
Amesema ili kupunguza upotevu wa umeme unaotokana na
kusafirisha umeme katika umbali mrefu pamoja na kuboresha ‘’stability mfumo”
nchi majirani Tanzania, Kenya na Ethiopia zimeingia makubaliano ya kuuziana
umeme pale ambapo nchi moja itakapokuwa na uhitaji kwa sababu za kupunguza
gharama pamoja na kuimarisha mfumo wake wa Gridi ya Umeme.
“Kwa kuwa vyanzo vyetu vya uzalishaji umeme vipo zaidi
upande wa Kusini kwenye Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa na Pwani kwa
sasa, jitihada mbalimbali zinafanywa ili kuimarisha hali ya umeme upande wa
kanda za Ziwa, Kaskazini Magharibi, pamoja na Kanda ya Kaskazini,” amesema
Mhandisi Mramba.
Ameeleza jitihada zinazoendelea ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa njia kubwa za kusafirishia umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma (400kV Chalinze- Dodoma) ili kupunguza upotevu wa umeme na kuimarisha mfumo wa Gridi.
Vilevile njia nyingine ni kuwa na chanzo nafuu cha umeme
kinachopatikana jirani na kanda hizi ambapo kwa sasa inaonekana kuusafirisha
umeme wa kutoka nchi jirani ni nafuu kuliko kusafirisha umeme katika umbali
mrefu ndani ya nchi.
Amesema katika kuhakikisha nchi zinazounda Ukanda wa
Mashariki (EAPP) zinatumia vyanzo mbalimbali vya umeme vya bei nafuu vilivyopo
kwenye ukanda huo, Nchi wanachama zimejiunga na soko la pamoja la kuuziana
umeme ambapo kutokana na vyanzo vilivyopo nchi inaweza kuuza au kununua umeme
wa bei nafuu kutoka kwenye nchi wanachama ili kupunguza gharama za uzalishaji.
“Kwa upande wa Kusini mwa Afrika Tanzania imejiunga na Soko la pamoja la (SAPP) ambapo tayari lilishaazishwa na linafanya kazi kwa nchi ambazo tayari miundombinu ilishakamilika ambapo kwa sasa tunaendelea na utekelezaji wa Mradi wa TAZA ambao kukamilika kwake kutaifanya Tanzania kutumia fursa ya umeme wa unaozalishwa kwenye Bwawa la Julius Nyerere na vyanzo vingine na kuanza kuuza umeme ukanda wa kusini mwa Africa (SAPP),” amesema Mhandisi Mramba.
“Hivyo lengo kuu la kuuza au kununua umeme ni kuimarishwa
kwa mifumo ya Gridi za Umeme za nchi husika pamoja na kupunguza gharama. Kwa
kutumia nafasi tuliyonayo kijiografia, Tanzania itatumia nafasi ya masoko haya
ya umeme kununua na kuuza umeme wa bei nafuu kutoka ukanda wa Mashariki mwa
Afrika na ukanda wa kusini mwa Afrika.”
Mhandisi Mramba amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea kuhakikisha kunakuwepo na miundombinu imara itakayowezesha manunuzi na mauziano ya umeme ndani ya ukanda wa EAPP pamoja na ukanda wa SAPP ili Tanzania inufaike kwa kuuza na kununua umeme lakini pia kuingiza fedha zitokanazo na gharama za kupitishia umeme kutoka ukanda mmoja kwenda mwingine.

0 Maoni