Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi
wa RISE inaendelea kuboresha miundombinu kwa kuondoa vikwazo katika maeneo
mbalimbali na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Mhandisi wa TARURA wilaya ya Arumeru ambaye pia ni msimamizi
wa mradi, Mhandisi Mohamed Bakari ameeleza kuwa mradi huo unajumuisha ujenzi wa
boksi kalavati (1), barabara Km. 1 na
ujenzi wa mitaro mita 800.
Amesema mradi huo wa unaondoaji vikwazo umesaidia wananchi
kufanya shughuli zao wakati wote na kufungua fursa za kiuchumi.
Naye, Bw. Simon Jeremia mkazi wa Ngaramtoni ameeleza kuwa
wakati wa mvua walikuwa wakipata shida kuvuka kwenda kwenye shughuli zao za
kila siku.
"Wakati wa mvua nyingi tuliteseka na mafuriko hasa sisi
bodaboda tulikuwa tukishusha wateja njiani, lakini kwa sasa mradi huu
ukikamilika tutafanya biashara muda wote,” amesema.
Aidha, Bi. Elizabeth Munuo mkazi wa Tarakwa ameishukuru Serikali kupitia TARURA
kwa ujenzi wa kalavati hilo ambalo limekuwa kiunganishi kati ya kata ya Tarakwa, Ngaramtoni na Elboro.
“Awali tulipata adha kubwa kuvuka hasa wakati wa mvua, lakini sasa tunaona daraja limekaribia kukamilika, tunaishukuru serikali kwa kutatua changamoto hii na kurahisisha ufanyaji wa shughuli zetu za kila siku.”


0 Maoni