Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imedhamiria kukuza sekta ya madini kwa kuhakikisha madini yanachakatwa na kuongezwa thamani hapa nchini badala ya kusafirishwa yakiwa ghafi. Hatua hii inalenga kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa, kukuza uchumi wa nchi na kulinda ajira za Watanzania.
Amesema hayo jana
Machi 25, 2025, jijini Dodoma wakati wa hafla ya kusaini Hati ya Makubaliano
(Memorandum of Understanding – MoU) kati ya Wizara ya Madini kupitia Kituo cha
Jemolojia Tanzania (TGC) na Kampuni ya Sunset Gem kutoka Thailand.
Mhandisi
Samamba amesema kuwa, makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa
kuhakikisha Tanzania inakuwa na uwezo wa kuongeza thamani madini ya vito badala
ya kuyauza yakiwa ghafi.
Aidha, amesisitizakuwa,
kupitia makubaliano hayo, Tanzania itanufaika na uhaulishaji wa teknolojia mpya
ya uongezaji thamani madini sambamba na kuboresha uwezo wa Kituo cha Jemolojia
Tanzania (TGC), ambacho ni taasisi muhimu katika sekta ya madini ya vito.
Aidha,
ameongeza kuwa Serikali inajenga jengo la ghorofa nane jijini Arusha kwa ajili
ya kuimarisha kituo hicho na kuonesha dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira
ya biashara ya madini ya vito nchini.
“Tunataka
kuhakikisha kuwa madini yetu hayauzwi ghafi, bali yanaongezwa thamani hapa
nchini ili kuyawezesha kuchangia kikamilifu katika uchumi wetu. Hatua hii pia
inalenga kuhakikisha ajira za Watanzania zinabaki ndani ya nchi kwa kuongeza
wataalamu wa ndani katika tasnia ya madini ya vito,” amesema Mhandisi Samamba.
Kwa upande
wake, Mtendaji wa Kampuni ya Sunset Gem kutoka Thailand, Pukkapon Piantumdee,
amesema kuwa kampuni yake imebobea katika ukataji, ung’arishaji na utambuzi wa
vito, na wanatarajia kutumia fursa hiyo kushirikiana na Tanzania katika
kubadilishana uzoefu na utaalamu.
Naye, Kaimu
Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Mhandisi Ally Maganga, amesema
kuwa hatua hiyo itawapa fursa vijana wa Kitanzania na wanafunzi wa kituo hicho
kwenda kujifunza zaidi nchini Thailand, pamoja na kupata ujuzi wa kisasa katika
teknolojia ya uongezaji thamani madini.
Hatua hiyo
inadhihirisha azma ya Serikali kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inafikia lengo
la kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa, hivyo ushirikiano na mataifa
yaliyoendelea katika sekta hii, kama Thailand, ni hatua muhimu katika
kufanikisha azma hiyo.


0 Maoni