Katika kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa, serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imegawa miche 5,000 ya miti kwa shule za sekondari Lake Eyasi, Diego na Lostete wilayani Karatu. Hatua hii inalenga kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuongeza thamani ya misitu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Miche
iliyotolewa inajumuisha aina mbalimbali za miti, ikiwemo Acacia spp, Senna
siamea, Acrocarpus fraxinifolius, Grevillea robusta, Spathodea campanulata,
Pinus patula, Jacaranda mimosifolia, Mangifera indica na Citrus sinensis.
Akizungumza jana Machi 20, 2025, wakati wa ugawaji huo, Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Karatu,
Mussa Kaisoy, alisema mpango huu unalenga kuwahamasisha wanafunzi na jamii kwa
ujumla kushiriki katika upandaji miti na matumizi endelevu ya rasilimali za
misitu.
“Upandaji wa
miti si tu unasaidia kuhifadhi mazingira, bali pia unachangia kuimarisha sekta
ya misitu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema Kaisoy.
Aidha, Kaisoy
alieleza kuwa miche hiyo inapatikana bure kwenye bustani ya miche iliyoko
katika jengo kuu la Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, ambapo wananchi
wanahamasishwa kuchukua na kupanda miti.
“Mpango huu
ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha kila wilaya inapanda angalau miti
1,500,000, huku TFS Karatu ikiwa imeotesha miche 75,000 kwa ajili ya taasisi za
umma na wananchi binafsi,” aliongeza.
Baadhi ya
walimu na wanafunzi waliopokea miche hiyo waliishukuru serikali kwa mpango huo,
wakisema utaboresha mandhari ya shule zao na kuwahamasisha kushiriki katika
utunzaji wa mazingira.
“Tunashukuru
kwa msaada huu wa miche. Tutahakikisha inakua na kuleta manufaa kwa vizazi vya
sasa na vijavyo,” alisema Daniel Kalai Laiza, Mkuu wa Shule ya Sekondari
Lostete.
Shughuli hii
imefanyika kwa ushirikiano wa viongozi wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa
Wilaya ya Karatu, Mheshimiwa Dadi Kolimba, pamoja na Mkurugenzi wa Wilaya ya
Karatu (DED), ambao walitoa msukumo mkubwa katika kuhakikisha miche hiyo
inagawiwa kwa wakati mwafaka wa mvua.
Mpango huu ni
sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Siku ya Misitu Duniani 2025:
“Ongeza
Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali kwa Kizazi Hiki na
Kijacho.”
0 Maoni