Mwenyekiti wa
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),
Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis R. Semfuko, amesema kuwa juhudi za Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta matokeo chanya katika kukuza sekta ya utalii
nchini. Hali hiyo imeonekana kwa ongezeko la idadi ya watalii na mapato katika
Hifadhi ya Mpanga/Kipengere, iliyopo katika mikoa ya Mbeya na Njombe.
Semfuko
aliyasema hayo Machi 19, 2025, alipotembelea Hifadhi hiyo kwa ziara ya kikazi
yenye lengo la kujionea vivutio vya utalii na kukagua miradi ya kimkakati ya utalii inayotekelezwa katika
hifadhi hiyo.
"Awali,
Hifadhi hii haikuwa na watalii kabisa. Hata hivyo, mafanikio makubwa yalianza
kuonekana kuanzia mwaka 2022, jambo ambalo linatokana na fedha zilizotolewa na
Serikali yetu chini ya uongozi wa Mama Samia," alisema Semfuko.
Aidha,
Semfuko aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne, TAWA imefanikiwa kujenga
miundombinu na kuweka vielelezo mbalimbali ambavyo vimesaidia kuvutia watalii
katika eneo hilo.
Meja Jenerali
(Mstaafu) Hamis Semfuko alieleza kuwa TAWA imetangaza fursa za uwekezaji katika
hifadhi hiyo na matarajio yake ni kupata
uwekezaji mkubwa katika sekta ya malazi na shughuli mbalimbali zitakazochochea
utalii na kufanya hifadhi hiyo kuwa kitovu cha utalii katika ukanda wa nyanda
za juu kusini.
Kwa upande
wake, Kamanda wa Hifadhi ya Mpanga/Kipengere, CI Donacian Makoi, alisema kuwa
kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, idadi ya watalii
wanaotembelea hifadhi hiyo imeongezeka kwa kasi kubwa. Kwa sasa, kila mwezi
hifadhi hiyo hupokea watalii kati ya 300 na 400, tofauti na awali ambapo
walikuwa wakipokea watalii kati ya 100 na 200 kwa mwezi.
kuhusu
mapato, katika kipindi cha kuanzia Julai
2024 mpaka Februari 2025 hifadhi hiyo imeingiza kiasi cha shillingi Millioni
155 tofauti na awali kabla ya uboreshaji wa miundombinu ambapo hifadhi
haikuweza kuingiza kiasi chochote cha fedha.
Makoi
aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2024/2025, TAWA inaendelea na miradi
miwili mikubwa ya kitalii ndani ya hifadhi hiyo. Miradi hiyo ni pamoja na
ujenzi wa sehemu za wageni kupata vyakula na vinywaji, maarufu kama "Tourism
Lounge," na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 30 kuelekea ukanda
wa juu wa hifadhi, hasa katika eneo la bustani ya dunia lenye spishi zaidi ya
400 za maua.
Naye, mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Prof. Jafari Kideghesho, alitoa rai kwa Watanzania kuwa na utamaduni wa kuthamini vitu vyetu na kuwahamasisha kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini hususan Hifadhi ya Mpanga/Kipengere.
Na. Beatus
Maganja- Mbeya



0 Maoni