WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua
umuhimu wa kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kama njia
mojawapo ya kuimarisha ustawi na kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha
jamii ya Watanzania inaishi kwa umoja na mshikamano kati ya wanaume na wanawake
na kuwa wote wanapata huduma za msingi kwa haki na usawa katika nyanja zote
ikiwemo kisheria, elimu, afya, uchumi na nafasi za maamuzi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 6, 2025)
alipozungumza na wananchi katika Kongamano la Wanawake Kanda ya Kusini ikiwa ni
sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika
Kitaifa Machi 8, jijini Arusha. Kongamano hilo limefanyika katika viwanja vya
Maegesho, Nachingwea mkoani Lindi.
Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuwawezesha wanawake
kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi Serikali imeendelea kutenga
asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri na kutoa mikopo kwa wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu. Mikopo hiyo imewawezesha wanawake kutekeleza
miradi kwa lengo la kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na pato la Taifa kwa
ujumla.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuiagiza
mikoa yote nchini iandae mkakati na mpangokazi wa utekelezaji maazimio ya
maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa mwaka 2025 ili uwe msingi wa
tathmini baada ya miaka mitano ya utekelezaji.
“Wanawake endeleeni kuhamasishana kutumia fursa za uwepo wa
madirisha yenye huduma za mikopo kwa wanawake kujikwamua kiuchumi. Nendeni
kwenye benki zinazotoa huduma hizo zilizoko karibu nanyi mpate mikopo hiyo
inayotolewa kwa masharti nafuu na hakikisheni mnarejesha kwa wakati mikopo yote
mnayopata, ili wananchi wengine waweze kukopa.”
Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Makundi Maalumu, Amon Mpanju alisema Wanawake ni muhimili na chachu
kubwa ya kuleta maendeleo katika ngazi ya familia na Taifa kwa ujumla, hivyo
kongamano hilo linalenga kuweka mikakati ya kuendelea kumkwamua mwanamke
kiuchumi.
Pia, Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa rai kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.”Wakati ukifika wanawake jitokezeni kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ili mshiriki katika kutoa maamuzi.”
0 Maoni