Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Rashal
Energies, Farhiya Warsame ambayo inajenga Bomba la Gesi kutoka Kisemvule hadi
Mbagala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG) na viwanda.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam tarehe
Machi 6, 2025 kando ya Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAPCE’25) linalofanyika kwa
siku tatu jijini Dar es Salaam.
Dkt. Biteko amesema kuwa lengo la Serikali ni kuwa na
mtandao mkubwa wa mabomba ya gesi pamoja
na vituo vya kujazia gesi kwenye magari ili kuwawezesha wananchi kupata huduma
kwa urahisi.
Kutokana na hilo Dkt. Biteko ameeleza kuwa Serikali ipo
tayari wakati wowote kutoa ushirikiano kwa kampuni zinazotaka kuwekeza kwenye
kutoa huduma hiyo kwa wananchi.
Kwa upande wake, Bi.Farhiya Warsame amemshukuru Dkt. Biteko
kwa miongozo yake ambayo imepelekea kampuni hiyo kuanza kutekeleza mradi huo.
Ameeleza kuwa wananchi wameonesha mwamko mkubwa kwenye
kuendesha vyombo vyao vya usafiri kwa kutumia gesi asilia badala ya mafuta
kutokana na gesi asilia kuwa na gharama nafuu kuliko mafuta.
Vilevile, Dkt. Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na
Mkurugenzi wa Kampuni ya Rock Mountain ya nchini Canada, Bw. Nick Lenstra
ambayo imesaini Mkataba wa Ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) kwa ajili ya kuanza kazi za upembuzi yakinifu na kuzungumza na
wadau wa ndani ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ili kutumia
gesi asilia kutengeneza nishati kwa njia ya kimiminika ambayo inaweza kutumika
kwenye ndege.
Hali kadhalika, Dkt.Biteko amekutana na kufanya mazungumzo
na Makamu wa Rais wa kampuni ya CNOOC kwa upande wa Uganda, Wang Juteng ambapo
pamoja kuzungumzia Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini, ameikaribisha
kushiriki Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu vya Mafuta na Gesi Asilia nchini.
0 Maoni