Mkakati wa Nishati Safi ya kupikia chini ya uasisi wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umeendelea
kupigiwa chapuo ambapo Korea Kusini imesema iko tayari kuunga mkono jitihada
hizo.
Hayo yamebainika leo Machi 6, 2025 katika mazungumzo ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko na Balozi wa Korea
Kusini nchini Tanzania, Mhe. Ahn Eunju kando ya Mkutano wa Mafuta na Gesi kwa
nchi za Afrika Mashariki unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema Tanzania imepiga hatua katika kuwezesha wananchi kupata unafuu
wa maisha kwa kupata na kutumia nishati safi na hivyo kuepukana na madhara
yanayotokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi yakiwemo magonjwa na vifo.
Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia wa miaka 10
unakusudia kuwawezesha asilimia 80 ya watanzania kuwa watumiaji wa nishati safi
ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
“Tunaendelea kutekeleza mkakati huu kwa kubadilisha mtazamo
wa watu waliokuwa wakitumia vyanzo vya asili vya nishati ambavyo sio salama,
lakini tunaendelea kubadili mitazamo yao ili waweze kuungana na jitihada hizi
za kitaifa na kimataifa za matumizi ya nishati safi ya kupikia.” amesema Dkt.
Biteko.
Amesema kuna jitihada mbalimbali kimataifa ikiwemo kusainiwa
kwa makubaliano kuhusu matumizi ya nishati kwa lengo la kuwezesha upatikanaji
wa nishati safi kwa gharama nafuu.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na
Sekta binafsi hauepukiki ili kufikia malengo yaliyokusudiwa
“Katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi Barani Afrika tulisaini
makubaliano kadhaa ikiwa ni pamoja na kupata fedha ili kuwawezesha wahitaji
kuboresha maisha yao kupitia Nishati Safi,” amesema Dkt. Biteko na kuongeza
kuwa Afrika inakusudia kuwawezesha watu milioni 300 kati ya milioni 600 Afrika
hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara hawana umeme.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Eunju amesema Serikali
yake imekuwa ikifuatilia kwa karibu kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Nishati
Safi ya Kupikia ambao ni muhimu sana kwa maendeleo ya ustawi wa jamii.
“Serikali yetu inaunga mkono ajenda hii ya nishati safi
inayobebwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambayo ni muhimu sana kuendelea
kutekelezwa kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Nishati,” amesema Balozi Eunju.
Pia amesema maeneo mengine ya kipaumbele ni sekta ya elimu,
maji na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
0 Maoni