Serikali imedhamiria kuboresha Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuijenga upya ili kuwezesha huduma zote kutolewa ndani ya jengo moja litakalokuwa na vitanda 1,757 kutoka 1,435 vya sasa ambapo mradi huo utagharimu USD .468 Mil (takribani TZS. 1.2 Trilioni) ambapo kati ya fedha hizo USD.364 Mil zitatoka Korea Kusini na Serikali ya Tanzania itachangia USD. 104 Mil.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt.
Rachel Mhaville kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH wakati akitoa taarifa
kwa umma juu ya mafanikio ya kipindi cha miaka minne chini ya uongozi wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa kwa sasa
upembuzi yakinifu wa mradi huo umekamilika hivyo hatua mbalimbali za kusaini
mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Korea zinaendelea vizuri.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni wa awamu moja
ambao utachukua miaka mitano kukamilika baada ya kusaini mkataba, hatua hii
haitaathiri utoaji wa huduma hospitalini hapa hivyo huduma zitaendelea kutolewa
kama kawaida.
“Utekelezaji wa mradi huu wa kihistoria katika sekta ya afya
nchini na Ukanda wa Afrika, utakua na faida lukuki ikiwemo kuboreshwa kwa
huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kupitia vifaa tiba vya kisasa na kwamba
Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha kusafirisha wagonjwa
nje ya nchi, kuwezesha wagonjwa kupata huduma zote katika eneo moja, kupunguza
mizunguko na usumbufu pamoja na kuwa na mpangilio mpya wa hospitali huku eneo
kubwa likibaki wazi kwa matumizi ya maendeleo mengine miaka 50 ijayo,” amesema
Dkt. Mhaville.
Hospitali ya Taifa Muhimbili yenye kampasi mbili ni Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini ina vitanda 2,043 ambapo Upanga kuna vitanda 1,435 na Mloganzila vipo 608.Katika kampasi zote mbili wagonjwa 4,000 wanaonwa kwa siku.
0 Maoni