Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa shilingi milioni 50 kwa ajili
ya maendeleo ya Shule ya Sekondari ya Seminari Uru, mkoani Kilimanjaro.
Mchango huo
umetolewa ili kuweka alama ya kumbukumbu ya kumuenzi marehemu Padri Canute Mkwe
Shirima AJ, aliyewahi kuwa Baba Gombera wa shule hiyo, mojawapo ya seminari
maarufu nchini.
Katibu Mkuu
wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, alitangaza mchango huo kwa niaba ya
Rais Dkt. Samia alipokuwa akitoa salaam za pole na rambirambi katika ibada ya
mazishi ya Padri Shirima, iliyofanyika Seminari ya Uru, Alhamisi, Machi 20,
2025.
“Haya yote
niliyoyasema hapa kumhusu Baba Gombera mstaafu Padri Canute Shirima, alivyokuwa
mlezi mzuri akifundisha nidhamu na uwajibikaji, nilimwambia Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nilimtaarifu
kuwa nakatisha ziara ili kuhudhuria mazishi haya. Mheshimiwa Rais akaniambia
anatoa shilingi milioni 50 kwa Seminari ya Uru ili mtengeneze jambo lolote
litakaloenzi heshima ya Padri Shirima,” alisema Balozi Nchimbi.
Akizungumzia
marehemu Padri Shirima, Dkt. Nchimbi, ambaye pia aliwahi kuwa mwanafunzi wa
seminari hiyo, alisema alikuwa mwalimu mahiri aliyesisitiza nidhamu na
uwajibikaji kwa wanafunzi wake.
Aliongeza
kuwa uongozi wa Padri Shirima ulisaidia Seminari ya Uru kupata sifa kubwa kwa kutoa
wahitimu waliodhihirisha uwezo mkubwa katika nyanja mbalimbali.
“Tunawashukuru
sana wazazi wa Padri Shirima kwa malezi mazuri waliyompa, ambayo nasi
tuliyapata kupitia yeye. Asanteni sana Mapadri Watume wa Yesu Kristo na mapadri
wote mliopo. Asante sana Baba Askofu Minde kwa heshima hii ya kuja kuongoza
ibada ya kumuaga mwalimu wetu,” alisema Balozi Nchimbi.
Akiongoza
ibada hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Askofu Rudovick Joseph
Minde ALCP/OSS, alisema marehemu Padri Shirima alikuwa zawadi ya Mungu kwa
jamii aliyowatumikia.
“Kwa namna
alivyoshuhudiwa hapa na umati huu uliokusanyika, mmeona na kusikia jinsi
alivyolea watu wakubwa sasa, wakiwemo maaskofu, mapadri, viongozi wa juu
serikalini, na hata tumepata salaam kutoka Ofisi ya Rais… Padri Canute alikuwa
zawadi ya Mungu kwetu,” alisema Askofu Minde.
Padri Canute
Mkwe Shirima, wa Shirika la Watume wa Yesu, ambaye alifariki akiwa katika utume
nchini Afrika Kusini, alizikwa kwa heshima zote za Kanisa Katoliki katika
makaburi ya Shule ya Sekondari ya Seminari Uru, Moshi, Kilimanjaro.
0 Maoni