WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi za kudhibiti viwango nchini zihakikishe uzalishaji wa bidhaa zote zinazozalishwa zikiwemo za afya zinakidhi ubora unaotakiwa na kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa.
Ametoa agizo
hilo leo (Alhamisi, Machi 20, 2025) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa
mitambo ya kuzalisha oksijeni kwa matumizi ya hospitali, ambapo amesisitiza
kuwa soko linatakiwa liwe na bidhaa salama, bora, na zinazokubalika kimataifa.
Mitambo hiyo inajengwa katika ofisi za TOL Gases, Temeke Dar es Salaam.
Amesema mradi
huo utakapokamilika utazalisha lita milioni 4.1 za oksijeni ya matibabu kwa
mwaka kuanzia mwaka 2026. “Hatua hii itaboresha upatikanaji wa oksijeni katika
hospitali na vituo vya afya, pamoja na kupunguza gharama za oksijeni ya
matibabu kwa asilimia 35 katika hospitali na vituo vya afya kote nchini, hivyo
kuimarisha huduma za afya kwa wananchi”.
Aidha, Waziri
Mkuu amesema mradi huu unaunga mkono juhudi endelevu za Serikali za kuhakikisha
oksijeni kwa ajili ya matibabu inapatikana kwa urahisi katika kila kituo cha
huduma za afya nchini.
“Mradi huu
utaongeza upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na zahanati nchini na
kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya kupumua ikiwa ni pamoja na kupunguza
vifo vya akina mama na kuokoa ya watoto wa Taifa hili.”
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godfrey Mollel amesema mradi huo ni muhimu kwa
sababu oksijeni inayozalishwa kwa njia hiyo inakuwa na viwango vya ubora, hivyo
itasaidia kuimarisha huduma za afya zitolewazo nchini pamoja na kupunguza vifo.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases, Daniel Warungu ametumia fursa hiyo kuipongeza
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kujidhatiti katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa
Watanzania.
Amesema
kampuni ya TOL inajivunia kushirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya
kuboresha huduma za afya, hususani upatikanaji na usambazaji wa gesi ya oksijeni
kwa ajili ya matibabu ukiwemo mradi wa shilingi bilioni 9.8 wa ufungaji wa
mifumo ya usambazaji gesi wodini katika vituo 129 vya huduma za
afya nchini kote.
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi mitambo ya kuzalisha oxygen kwa matumizi
ya hospitali, kwenye kampuni ya Tanzania Oxygen Limited (TOL), Temeke jijini
Dar es Salaam Machi 20, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akipokea Tuzo ya Umahiri na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania
Oxygen Limited (TOL), Daniel Warungu, baada ya kuweka jiwe la msingi mitambo ya
kuzalisha oxygen kwa matumizi ya hospitali, katika kampuni ya Tanzania Oxygen
Limited (TOL), Temeke jijini Dar es Salaam Machi 20, 2025. Kushoto ni Naibu
Waziri wa Afya Dkt. Godwin Molel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
0 Maoni