Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde leo
amekabidhi Kompyuta 50 na Printa 50 kwa Shule za Sekondari za serikali za
Dodoma Jiji pamoja na maabara ya kisasa ya Kompyuta kwa Shule ya Sekondari
Viwandani na kuahidi kuifanya Dodoma kuwa kinara kwenye matumizi ya teknolojia
kwenye kufundishia.
Mavunde ameyasema hayo leo katika hafla ya kukabidhi vifaa
hivyo iliyofanyika Shule ya Sekondari Viwandani.
“Tunaipongeza serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya miundombinu kwenye sekta ya elimu
Jijini Dodoma ambapo kwa mwaka huu wa fedha zimetengwa Tsh 16 bilioni. Kompyuta
hizi na Printa natumai zitachochea ufaulu na kuwajengea uwezo wanafunzi wetu.”
Katika Kompyuta hizi tumeweka mitihani yote ya kitaifa
kuanzia mwaka 1988-2024 kwa Kidato cha II, IV, VI na QT, vitabu vya ziada na
kiada, Simulation za masomo ya Sayansi, video tutorials za masomo mbalimbali na
notes za masomo yote,” alisema Mavunde.
Naye Mkuu wa Wilaya wa Dodoma Mh. Alhaj Jabir Shekimweri
amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Mbunge Mavunde kwenye sekta ya Elimu na
kuitaka Halmashauri ya Jiji Dodoma kuhakikisha inatenga fedha ili kuziunganisha
shule zote za Dodoma na Intaneti.
Diwani wa kata ya Viwandani Mh. Jaffar Mwanyemba amemshukuru Mbunge Mavunde kwa ukarabati na kuweka vifaa vya maabara na kuwataka wanafunzi watumie nafasi hiyo kujiongezea maarifa zaidi.
0 Maoni