Tanzania inashiriki katika
msafara wa kunadi vivutio vya utalii katika nchi za Ulaya Magharibi
ulioanza tarehe 10- 15 machi 2025 ambapo wauzaji na wanunuzi katika sekta ya
utalii wanakutana katika msafara huo wenye mawakala zaidi ya 50.
Msafara huo unaojulikana kwa jina la "My Tanzania
Roadshow 2025 " na kuratibiwa na kampuni ya Kili Fair unafanyika katika
miji mitano ya Cologne Ujerumani, Antwerp Ubelgiji, Amsterdam Uholanzi, London
na Manchester iliyopo nchini Uingereza kunadi vivutio vya Utalii vilivyopo
Tanzania ambapo nchi za ulaya ni soko kubwa linaloleta Watalii wengi Tanzania .
Akizungumzia Msafara huo Mkurugenzi wa Masoko kutoka Bodi ya
Utalii Tanzania Ernest Mwamaja amesema kuwa Wadau na wauzaji wa Mazao ya utalii
ukihusisha vyama vya waendesha utalii, wamiliki wa hoteli, makampuni ya ndege kutoka Tanzania
wanakutana na wanunuzi wa Utalii
(Buyers) kwa ajili ya kufanya biashara.
Mwamaja ameeleza kuwa nchi ya Ujerumani pekee takribani
watalii 100,000 wanatembelea vivutio vya Utalii vilivyopo Tanzanka kila mwaka
ambapo kupitia misafara ya utalii muitikio wa wadau kushiriki umeendelea
kuongezeka kila mwaka.
"Kupitia Misafara hii hasa katika soko la Ulaya
magharibi tutaendelea kuwashawishi wageni kuja Tanzania kwa wingi ili tuongeze
pato la Serikali, na tunaamini jitihada za kuboresha miundombinu ya utalii
zinazoendelezwa na Serikali ya awamu ya sita zitachangia wageni wanaokuja nchini
kwetu kukaa siku nyingi zaidi kwa kuwa tuna mtawanyiko wa vivutio vya Utalii
katika maeneo mengi" ameeleza Mwamaja.
Katika Msafara huo unaoshirikisha kampuni za Sekta binafsi zaidi ya 50 unajumuisha pia taasisi za Serikali ambazo ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) na shirika za Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambazo ushiriki wao unatoa hakikisho kwa sekta binafsi kuwa Serikali inawaunga mkono jitihada zao kwa kuweka mazingira rafiki, kuboresha miundombinu na huduma za utalii kwa wageni wanaotembelea Tanzania.




0 Maoni