Urusi imesisitiza tena dhamira yake ya kuimarisha uhusiano
wa kisayansi, utafiti na elimu na Tanzania katika sekta za mazingira na
teknolojia, huku ujumbe wa wajumbe kumi kutoka Urusi ukiwa nchini kama sehemu
ya Msafara wa Kisayansi na Kielimu wa Urusi na Tanzania.
Akizungumza mapema leo, Machi 10, 2025 katika Kituo cha
Utamaduni cha Urusi jijini Dar es Salaam, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe.
Andrey Avetisyan, alielezea fursa kubwa zilizopo kwa ushirikiano katika misitu,
kilimo, na uhifadhi wa wanyamapori.
"Tanzania ina zaidi ya hifadhi 22 za taifa, nyingi kati
yake hazijajulikana sana kimataifa. Zaidi ya Serengeti na Ngorongoro, kuna
mandhari za kipekee ambazo wachache wameziona. Kuna nafasi kubwa ya
kushirikiana katika uhifadhi wa mazingira," alisema.
Ujumbe huo wa Urusi, ukiwahusisha wasomi na watafiti, upo
nchini ili kuangaza furs za ushirikiano wa kisayansi, programu za kubadilishana
wanafunzi, pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta za misitu na kilimo.
Balozi Avetisyan alibainisha kuwa wahitimu wa vyuo vikuu vya
Urusi tayari wanachangia katika juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini
Tanzania, hususan katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Afrika
(Mweka).
Mratibu wa Ugeni huo, Mhifadhi Jared Otieno kutoka Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS),, aliukaribisha ujumbe huo wa Urusi na kuelezea
furaha yake kuhusu ushirikiano huo uliosubiriwa kwa muda mrefu katika usimamizi
wa misitu na uhamishaji wa teknolojia.
"Tumefarijika sana kuwa wenyeji wenu hapa Tanzania
tunapokamilisha ushirikiano huu muhimu. Sekta ya misitu inapanuka, lakini
changamoto bado ni nyingi, hasa katika upande wa teknolojia. Uwepo wenu hapa ni
hatua kubwa kwetu," alisema Otieno.
Alisisitiza umuhimu wa teknolojia za kisasa kusaidia
mashamba ya miti yanayomilikiwa na sekta binafsi pamoja na Serikali na
kuhakikisha rasilimali za misitu zinachangia kikamilifu katika uchumi wa
taifa.
Otieno alieleza ratiba ya ujumbe huo, ambao unajumuisha
ziara katika miji ya Dodoma, Arusha, na Moshi, ambako watakutana na maafisa wa
serikali, taasisi za utafiti, na jamii za wenyeji. Timu hiyo pia itatembelea
Hifadhi ya Ngorongoro ili kujifunza jinsi uhifadhi wa wanyamapori, mifugo, na
utamaduni wa kiasili wa Wamasai unavyoweza kuunganishwa kwa njia endelevu.
"Hatulengi tu misitu, bali pia uhifadhi wa mifumo ya
ikolojia na jinsi teknolojia inavyoweza kusaidia katika uendelevu wake.
Ushirikiano huu lazima uendane na mikakati ya kimataifa ya mazingira ili
kuhakikisha mafanikio yake ya muda mrefu," aliongeza.
Ziara hii inatarajiwa kufungua milango kwa miradi mipya ya
utafiti, programu za kubadilishana wanafunzi wa vyuo vikuu, na miradi ya pamoja
ya kisayansi, hatua ambayo itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Urusi
na Tanzania.



0 Maoni