Ujumbe wa wataalam kutoka jamhuri ya Cuba wakiambatana
watalaam wa uhifadhi kutoka Wizara ya Maliasilii na Utalii wametembelea bonde
la kreta lililopo Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kuona hali halisi
ya uwepo wa mimea vamizi ndani ya Bonde hilo.
Akizunguza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika leo Februari
18, 2025 Dkt. John Bukombe Kutoka taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania
(TAWIRI) amesema lengo la ziara hiyo ni hatua za awali za kutafuta namna ya
kukabiliana na changamoto ya mimea vamizi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.
"Watalaam hawa tutasaidiana kutafuta namna ya
kukabiliana na changamoto ya mimea vamizi inayoathiri uoto wa asili ndani ya
bonde la Kreta ambayo kwa kiasi kubwa imesababisha kutoweka kwa mimea asili
ambayo ni malisho ya wanyamapori," alisema Dkt. Bukombe.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Kitengo cha Usimamizi wa
Wanyamapori na Utafiti, Afisa Uhifadhi Mkuu Lohi Zakaria amesema kuwa NCAA
imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kudhibiti mimea vamizi ndani Eneo la
Hifadhi ambapo hata hivyo jitihada hizo bado hazijazaa matunda yaliyotarajiwa.
"NCAA tumekuwa tukijitahidi kudhibiti mimea hii kwa
kufyeka na kulima njia ambazo hazijaleta mafanikio, tunaamini kwamba ujio wa
wataalam hawa ni mwanzo mzuri wa kufikia suluhisho la kudumu," alisema
Lohi.
Dkt. Orlando Enrique Sanchez Leon ambaye ni mkuu wa ujumbe
wa wataalam kutoka Cuba alieleza kuwa wameona tatizo la kuwepo kwa mimea vamizi
ndani ya bonde la kreta ambapo pamoja na sababu zingine mwingiliano wa shughuli
za binadamu na Wanyamapori unaweza kuwa chanzo cha uwepo wa mimea hiyo hifadhi
hapo.
Hata hivyo, Dkt. Orlando alisisitiza kuwa wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wataalam wake kuhakikisha kuwa kutapatikana mbinu bora za kuthibiti mimea hiyo vamizi ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa.
0 Maoni