Mkuu wa Mkoa wa Kigoma (RC), Thobias Andengenye jana Februari 25, 2025 amezindua ulipaji fidia kwa wakazi wa vitongoji vya Mahasa na Kabuyungu katika kijiji cha Kalilani, kata ya Buhingu wilayani Uvinza, Kigoma.
Wananchi wa kata ya Buhingu wanatakiwa kuhama kupisha eneo
lenye ukubwa wa ekari 20 kwa ajili ya ikolojia ya wanyamapori adimu aina ya
Sokwe walio hatarini kutoweka, ili waweze kuongezeka vizuri ndani ya Hifadhi ya
Taifa Milima ya Mahale.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ilifika katika kijiji cha Kalilani na
kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuwajali wananchi wake, ambapo shilingi bilioni 1.68 zitatolewa kwa
ajili ya kulipa fidia kwa wananchi hao.
"Serikali ina mipango mizuri kwa wananchi wake, haiwezi
kuwatoa hapa bila ya fedha mkapate shida muendako, fedha hizi zimekuja ili
kuwapa nguvu ya kuanza kule mlipopangiwa," alisema RC Andengenye.
Alifafanua kuwa serikali imekuwa ikilipa fidia katika maeneo
mengi nchini kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, hivyo kijiji cha
Kalilani na vitongoji vyake viwili sio eneo la kwanza kulipwa fidia.
"Leo tumekuja kuonesha kuwa serikali inayo dhamira ya
dhati, kwa wale ambao tayari wamefanyiwa tathmini, Serikali inayojali maisha ya
wananchi na kusimamia haki zote, ndio maana zoezi hili ni la wazi sio la
kificho, wataalamu wapo kujibu maswali yenu na kuwasaidia," Andengenye
aliwaambia wananchi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mhe. Dihah
Mathalani alibainisha kuwa sio wananchi wote wameridhia na kufanyiwa tathmini
kwani wapo waliokataa kwa sababu zao, hivyo alitoa rai kwa waliofanyiwa tathmini
kutokusikiliza uchochezi, kuvunjwa moyo na kupuuza uvumi unaosambaa kutoka kwa
baadhi ya wananchi wasiotaka uhamishwaji huo kufanikiwa.
"Serikali ina taratibu zake, na taratibu zote
zimefuatwa, hivyo tukae pamoja tusikilizane, tushirikiane ili zoezi liende
vizuri, hakuna jambo litaharibika tukiwa wamoja," alisisitiza.
Akifafanua zaidi, Afisa Mhifadhi Mkuu, Halid Jumanne Mngofi
ambaye ni Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Milima ya Mahale, alisema kati ya kaya
375 zilizotakiwa kufanyiwa tathmini, ni 205 zimeridhia kufanyiwa tathmini na
ziko tayari kulipwa fidia ziweze kuhama.
Eneo watakaloliacha ni muhimu kwa ustawi wa Sokwe
wanaopatikana Hifadhi ya Milima ya Mahale.
"Vitongoji hivi viwili vya Hamasa na Kabuyungu vipo
katika mwambao wa Milima ya Mahale na mwambao wa Ziwa Tanganyika, ambapo
mwingiliano wa wananchi umekuwa mkubwa na wananchi wanazidi kuongezeka, hii
italeta athari katika uhifadhi, ni vyema serikali imeliona mapema na kulifanyia
kazi," alisema Halid.
Kuimarika kwa mazingira asilia ya Hifadhi ya Taifa Milima ya Mahale kutawafanya Sokwe kuongezeka, na watalii wengi kumiminika, hivyo kuongeza pato la Taifa.





0 Maoni