Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema kuwa angependa kuona wananchi wa Kahama wanashirikiana na
kuungana kwa pamoja katika shughuli za maendeleo ya Wilaya yao.
Aidha, amewaasa kutoacha msingi wa Chama Cha Mapinduzi wa
kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba Taifa linategemea CCM iwahudumie na sio
kuruhusu mipasuko miongoni mwao.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Februari 25, 2025 Kahama, mkoani
Shinyanga wakati aliposhiriki katika Mkutano Maalum wa Chama Cha Mapinduzi
Jimbo la Msalala uliolenga kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025.
Akizungumzia fursa za maendeleo zilizopo wilayani humo, Dkt.
Biteko amesema kuwa Kahama ni
Wilaya ya kimkakati ambayo ina bandari
kavu iliyopo Isaka ambapo pia kitajengwa kiwanda cha kuchenjua madini pamoja na
uwepo wa barabara inayoounganisha nchi za maziwa makuu.
“ Kutokana na uwepo
wa fursa hizi tukishindwa kuungana tukashughulika na maendeeo ya watu basi
watatushangaa. Nataka nitoe wito, pendaneni, shikamaneni Mungu amewapa kila
aina ya utajiri tumieni fursa hiyo kujiletea maendeleo kwenye wilaya yenu na
msiruhusu mipasuko katika chama chetu,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “Nawaomba baada ya mkutano huu tutoke hapa
tukiwa wamoja na tuweke mbele maslahi ya Chama chetu na watu wetu,”
Pia, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Msalala, kwa kazi kubwa
aliyoifanya ya kuhakikisha wananchi wa Jimbo hilo wanapata miradi ya maendeleo
na hivyo kutatua changamoto walizokuwa nazo hapo awali.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amemshukuru Mhe. Rais
Samia kwa kutoa fedha nyingi katika Jimbo hilo ambazo zimetumika kutekeleza
miradi mbalimbali kama vile ya maji, elimu, afya na miundombinu.
“ Mhe. Rais Samia amefanya makubwa katika nchi yetu, leo
tunazungumza kuhusu miradi mingi na mikubwa hapa Kahama, tunazungumzia kujengwa
kwa barabara ya Kakola kwa kiwango cha lami. Amefanya uchimbaji madini ubaki
kwenye maendeleo yetu anataka uwepo wa miradi mingi zaidi ya barabara na maji
niwaombe tumuombee ili aendelee kutimiza haya kwa ajili ya Watanzania,” amesema
Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Mhe. Rais Samia bado ana dhamira ya dhati ya
kuhakikisha Watanzania wote wanapata maendeleo na kuishi katika mazingira bora
zaidi.
“ Wito wangu kwenu shikamaneni, pendaneni, vumilianeni
tukijenge Chama chetu ikiwa muda utafika wakati wa uchaguzi basi chagueni
anayefanya kazi mwacheni anayesema watu. Mhe. Mbunge Iddi endelea kuchapakazi
kwa maendeleo ya Jimbo lako,” amemalizia Dkt. Biteko.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Msalala lililopo Mkoa wa
Shinyanga, Mhe. Iddi Kassim Iddi wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa
Ilani ya CCM kwa Jimbo hilo kwa Mwaka 2020 hadi 2025 amempongeza Dkt. Biteko
kwa hatua ya kuendeleza sekta ya nishati kwa kusaidia vitongoji vyote vya
Jimbo hilo kupata umeme.
Serikali inaendelea na azma yake ya kusambaza huduma za
umeme katika vijiji vyote nchini. Hapa tumejulishwa kuwa Msalala ina jumla ya
vijiji 92, ambavyo vyote vimefikiwa na huduma ya umeme, kazi iliyobaki ni
kupeleka umeme katika vitongoji.
Akizungumzia sekta ya maji amesema mwaka 2020 hadi 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali mfano ametoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya miradi ya kusambaza
maji katika vijiji mbalimbali.
Ameendelea kusema mafanikio ya miradi hiyo imesaidia Jimbo
hilo ambalo kwa sasa wanaendelea kusambaza maji katika maeneo ambayo
hayajafikiwa na huduma hiyo hususan katika vitongoji na tayari Serikali
imeshaleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“ Wakati naingia madarakani miradi ya maji ilikuwa kwa
asilimia 25 pekee na sasa miradi ya maji imefikia asilima 95,” amesema Mhe.
Iddi.
Kwa upande wa sekta ya elimu amesema kuwa Rais Samia
ameboresha sekta hiyo kwa kutoa fedha zilizosaidia katika utekelezaji wa miradi
ya ujenzi wa madarasa, mabweni na maabara.
“ Tumekuwa na shule nyingi maana yake tutawasomesha watoto
wetu kwa kiwango cha kutosha, pia tumeanzisha ujenzi wa Chuo cha VETA na
kitakapo kamilika kitakuwa na manufaa makubwa kwa jamii hususan vijana ili
wapate ujuzi na kuajirika katika soko la ajira,” amesema Mhe. Iddi.
Halikadhalika katika sekta ya barabara amesema kuwa katika
kipindi cha miaka mitano Jimbo hilo kwa kushirikiana na TARURA wamefungua
barabara nyingi ikiwemo barabara inayotoka Kakola kwenda Kahama ambayo kwa sasa
inapitika vizuri. Aidha, amemshukuru
Rais Samia kwa kutekeleza Ilani ya CCM katika Jimbo hilo kwa asilimia 99.9.




0 Maoni