Balozi Tembele afanya mazungumzo na Rais wa Taasisi ya Indonesia ya DSI

 

Mapema leo, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mheshimiwa Macocha Moshe Tembele amekutana na kufanya mazungumzo na Prof. Sabela Gayo, Rais wa Taasisi ya Indonesia Dispute Board (DSI).

Mazungumzo hayo yalijikita zaidi kujadili kuhusu umuhimu wa kuanzisha Ushirikiano wa Kitaasisi kati ya Taasisi ya Indonesia Dispute Board (DSI) na Taasisi mbalimbali zinazohusika na uhamasishaji wa matumizi ya Njia Mbadala za Usuluhishi wa Migogoro (Alternative Dispute Resolution- ADR) zilizopo nchini Tanzania.

Aidha, Mheshimiwa Balozi alibainisha kuwa, kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia miaka ya hivi karibuni unaotokana na ukuaji wa biashara kati ya nchi hizo mbili pamoja na ongezeko la uwekezaji katika sekta za nishati, kilimo na mafuta na gesi kutoka Indonesia kuja nchini ni fursa muhimu ya kuanzisha ushirikiano katika eneo la usuluhishi wa migogoro ya kibiashara kati ya Tanzania na Indonesia.

Kadhalika, mbali na kupongeza hatua kubwa iliyopigwa na Taasisi ya Indonesia Dispute Board (DSI) katika kuhamasisha matumizi ya Njia Mbadala za Utatuzi wa Migogoro (ADR) nchini Indonesia na nchi mbalimbali duniani, Mheshimiwa Balozi aliiomba Taasisi hiyo kuanzisha ushirikiano na Tanzania utakaowezesha Taasisi  zinazojishughulisha na uhamasishaji wa matumizi ya Njia Mbadala za Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara zilizopo nchini kunufaika kupitia programu mbalimbali za kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo wataalamu wetu (mediators).

Vilevile, Mheshimiwa Balozi aliufahamisha ujumbe huo kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuhamasisha matumizi ya Njia Mbadala za Utatuzi wa Migogoro, na kutoa wito kwa Taasisi ya DSI kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia uzoefu walionao katika eneo la usuluhishi wa migogoro ya kibiashara kwa kuwajengea uwezo zaidi wataalamu wa kada husika.

Kwa upande wake Prof. Sabela Gayo, alikubaliana na masuala yote yaliyowasilishwa na Mheshimiwa Balozi na kumhakikishia kuwa, Taasisi yake ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na Taasisi zinazohusika na utatuzi wa migogoro ya kibiashara zilizopo nchini.

Mwisho, Mheshimiwa Balozi alimkaribisha Prof. Gayo na ujumbe wake kufanya ziara nchini ili kujifunza zaidi kuhusu mifumo mbalimbali ya usuluhishi inayotumika, na kukutana na wadau wote muhimu kama vile Serikali na Taasisi zinazohusika na usuluhishi wa migogoro ya kibiashara.

Indonesia Dispute Board (DSI) ni Taasisi ya kujitegemea inayojishughulisha na uhamasishaji wa matumizi ya Njia Mbadala za Usuluhishi wa Migogoro ya kibiashara (ADR) nchini Indonesia na nchi mbalimbali duniani. Taasisi hiyo yenye makao makuu yake Jakarta, Indonesia ina ubia na Vituo vya Kimataifa vya Usuluhishi (International Commercial & Arbitration Centers) kutoka katika nchi kumi na nane (18) zikiwemo Tanzania, Singapore, Malaysia, Denmark, Uturuki, Afrika Kusini, Thailand, China, Pakistani, Cambodia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Jamhuri ya Korea, Norway n.k.



Chapisha Maoni

0 Maoni