WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu imetumia shilingi trilioni 8.2 kugharamia wanafunzi tangu
ilipoanzishwa.
Amesema kuwa
pia katika kipindi hicho wanafunzi takribani 830,000 wamenufaika na mfumo huo
wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya mikopo.
Amesema hayo
leo Jumatatu (Februari 17, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu, iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, Dar es Salaam.
“Mafanikio
tuliyonayo leo, ni matokeo ya utashi wa kisiasa, uongozi thabiti, maono na
michango ya viongozi wetu. Viongozi wetu katika awamu zote walifanya kazi kubwa
ya kuhakikisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya vizuri,
viongozi wetu walioona mbali kuanzisha mfumo huu wa ugharimiaji wa elimu ya juu
kupitia Bodi ya mikopo.”
Aidha,
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
imefanikiwa kukusanya fedha kiasi cha shilingi trilioni 1.5 “Ninatambua
marejesho hayo yamepatikana kutokana na jitihada na ubunifu mkubwa ambao
unasaidia kuwafikia wanufaika ambao wamehitimu na mikopo yao imeiva.”
Ameongeza
kuwa katika kuhakikisha kuwa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu haiwi mzigo
kwa Wanafunzi, Serikali iliamua kufuta tozo za kulinda thamani ya fedha ili
kuondoa changamoto katika urejeshaji wa mikopo. “Kwa sasa mnufaika anarejesha
kiasi kile kile ambacho amekopeshwa kwani tozo hizo zilikuwa zinasababisha
ongezeko la madeni ya mikopo hiyo.”
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Bodi ya Mikopo kuendelea kuweka mikakati ya
kuendana na kasi ya mababiliko ya teknolojia na ifanye maboresho ya
kujiunganisha na kuzungumza lugha moja na taasisi za fedha nchini.
Kwa upande
wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa
wakati Rais Dkt. Samia anaingia madarakani alikuta fedha zinazotolewa kwa ajili
ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni shilingi bilioni 464. “Lakini
alipoingia aliagiza fedha kwa ajili ya mikopo ziongezwe, na tuliongeza hadi
kufikia bilioni 570, tukaendelea hadi bilioni 654 na sasa ni shilingi bilioni
731.”
Ameongeza
kuwa Rais Dkt. Samia katika kuhakikisha kada za Sayansi zinaendelea kupewa
kipaumbele ili kuzalisha wataalam wengi zaidi, aliiagiza Wizara ya Elimu
kutenga fedha kwa ajili ya kuanza kutoa ufadhili kwa ajili ya kada hizo ambayo
tuliita Samia Scholarship.
“Wakati
tunaanza tulitoa shilingi bilioni 3 kama majaribio, baadae tulitoa bilioni 6 na
sasa hivi tumetoa shilingi bilioni 8.9.”



0 Maoni