Waziri wa
Madini Mhe. Anthony Mavunde amepiga marufuku raia wa kigeni kuingia na kufanya
shughuli kwenye leseni za uchimbaji mdogo; hii ni kufuatia changamoto
zilizobainika katika uingiaji mikataba ya utoaji wa misaada ya kiufundi kati ya
wamiliki wa leseni ndogo za uchimbaji madini na raia wa kigeni. 
Amesema hayo
leo Februari 17, 2025 wakati akifungua Kikao Kazi cha kupokea maoni kutoka kwa
wadau kuhusu mapendekezo ya kuandaa Rasimu ya Kanuni za Madini za Utoaji Msaada
wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za Mwaka 2025
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Edema Hoteli Mkoani Morogoro.
Aidha, Waziri
Mavunde ametoa wito kwa washiriki wote wa Kikao Kazi hicho kutoa maoni yao kwa
uhuru na uwazi ili kusaidia upatikanaji wa Kanuni nzuri na inayotekelezeka kwa
lengo la kuongeza tija katika mnyororo mzima wa shughuli za Sekta ya Madini
nchini na kutekeleza sharti la kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini Sura Namba
123.
"Katika
kipindi cha muda mfupi tumeshuhudia mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Madini
kutokana na utashi wa Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatamani
kuona wachimbaji wadogo wanafikiwa, ambapo leo naagiza ofisi ya Kamishna
kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waweze kuhitimu kutoka hapo walipo na
kuendelea mbele."
"Haiingii
akilini, mgeni anakuja, anaingia kwenye leseni ya mchimbaji mdogo kupitia
mkataba wa utoaji msaada wa kiufundi, wachimbaji wadogo hawanufaiki wala
kuendelea zaidi kimatumizi ya teknolojia na mitaji, hili halikuwa lengo la
Sheria katika kuweka sharti hilo ili kuendeleza wachimbaji wadogo," alibainisha
Waziri Mavunde.
Pamoja na
mambo mengine, Waziri Mavunde ametoa onyo kwa wachimbaji wadogo kutowakaribisha
wageni bila kufuata utaratibu katika leseni za uchimbaji mdogo wa madini ambapo
itapelekea kufutiwa leseni kwa atakaye kiuka agizo hilo na kutoa angalizo kwa
Maafisa Madini Nchini kudhibiti uingiaji wa wageni bila kufuata taratibu.
Kwa upande
wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema Kikao hicho
kimelenga kupokea mapendekezo ya wadau kwa ajili ya kuandaa rasimu ya Kanuni za
Msaada wa Kiufundi kwa ajili ya wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo ambapo
Wizara iko huru na tayari kupokea maoni ya kila mdau.
Naye, Rais wa
Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini Tanzania John Bina amempongeza Waziri
Mavunde kwa uamuzi wa kuwashirikisha wadau wa Sekta ya Madini wakiwemo
wachimbaji wadogo ili kuandaa rasimu ya Kanuni hizo kuliko kujifungia na
kuandaa Wizara pekee.
Kikao hicho
kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Wachimbaji Wadogo kutoka
mikoa yote nchini, vyama vya wachimbaji wadogo wanawake Tanzania na
wafanyabiashara wa madini nchini.


 
 
 
 
 
 
 
 
0 Maoni