Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na Uhalifu, Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki (UNODC ROEA), imejipanga kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kudhibiti uhalifu unaoathiri mazingira (Enviromental Crimes) na kulinda bayoanuwai.
Hayo yamejiri
leo Februari 17, 2025 katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) na Mwakilishi wa Kanda wa Ofisi ya Umoja wa
Mataifa ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na Uhalifu, Ofisi ya Kanda ya Afrika
Mashariki (UNODC ROEA), Bi.Ashita Mittal, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
katika kikao hicho, Mhe. Chana amesema kupitia kikao hicho Wizara ya Maliasili
na Utalii na UNODC wamepata fursa ya kuangalia jinsi UNODC inavyounga mkono
jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kukabiliana na
uhalifu unaoathiri mazingira, kuangazia miradi inayoendelea, ikiwa ni pamoja na
usafirishaji haramu wa nyara na mazao ya misitu, uvuvi haramu na usalama wa
baharini.
Pia, Mhe.
Chana ametumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa UNODC kwa msaada wa
kifedha na kiufundi uliotolewa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya
kupambana na uhalifu unaovuka mipaka (Transnational Organized Crimes) ikiwemo
Biashara Haramu ya Nyara(IWT) kupitia Kitengo cha Udhibiti wa pamoja kilichopo
Bandari ya Dar es Salaam (Joint Port Control Unit – JPCU).
“Biashara
Haramu ya Wanyamapori sio tu inaleta tishio
kwa usalama wa rasilimali za wanyamapori na misitu miongoni mwa nchi wanachama,
hivyo kuathiri uchumi wetu na kuwezesha uhalifu mwingine wa kupangwa kama vile
utakatishaji fedha na ugaidi,” Mhe. Chana amesisitiza.
Kwa upande
wake, Bi.Ashita Mittal ameahidi kuwa UNODC itaendelea kushirikiana na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka
mipaka kwa kutoa zaidi mafunzo katika nyanja mbalimbali na vitendea kazi
kupitia programu mbalimbali zitakazoandaliwa na pande zote mbili.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Maafisa kutoka UNODC na Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Na. Happiness
Shayo - Dar es Salaam
0 Maoni