Buruhani awataka vijana kukataa mkumbo wa machafuko na kukimbilia fursa za Samia

Na Mwandishi Wetu

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhani, ametoa mwito mzito kwa vijana nchini kote kusimama imara kama walinzi wa amani na utulivu, huku akiwaonya vikali kujiepusha na makundi yenye nia ovu yanayoshawishi jamii kuvunja sheria na kuhatarisha usalama wa taifa.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika kata mbalimbali mkoani hapa wakati wa mwendelezo wa Operesheni ya Vijana Daka Fursa na Samia yaani VIDAFUSA Awamu ya Pili, Buruhani alisema kuwa amani na mshikamano ndio nguzo pekee zinazowezesha nchi kupiga hatua za kimaendeleo, hivyo vijana hawapaswi kukubali kufuata mkumbo unaolenga kuichoma moto nchi na kubomoa yaliyojengwa.

Kiongozi huyo wa vijana alifafanua kuwa ustawi wa kiuchumi na kijamii unaoshuhudiwa hivi sasa katika sekta mbalimbali nchini unahitaji ulinzi wa hali ya juu kutoka kwa nguvu kazi ya taifa, na kuwataka vijana kutambua kuwa wana nafasi ya msingi sana katika kujenga au kubomoa mustakabali wa Tanzania.

Buruhani alisisitiza kuwa badala ya vijana kupoteza muda na nguvu zao kwenye majukwaa yanayochochea chuki, fujo na mifarakano, wanapaswa kukimbilia na kuzichangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo mikopo ya uwezeshaji, elimu ya ujasiriamali na programu maalumu za kukuza vipaji na uchumi wao.

Aliongeza kuwa operesheni hiyo ya VIDAFUSA itaendelea vijijini na mijini mkoani Kagera ili kuwajengea vijana uwezo wa kujikwamua kiuchumi na kuwapa elimu ya uzalendo ili wasiweze kushawishiwa kirahisi na watu wanaotaka kuvuruga utulivu wa nchi kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa na kijamii.

Chapisha Maoni

0 Maoni