Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Cuba zimekubaliana kushirikiana
katika maeneo ya utalii na uhifadhi wa wanyamapori hasa kukabiliana na
changamoto ya mimea vamizi ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa.
Hayo yamejiri
jana Februari 16, 2025 katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam ambapo
ujumbe wa Cuba uliongozwa na Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Cuba, Mhe.
Humphrey Polepole na Balozi wa Jamhuri ya Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis
Despaigne Vera na kwa Tanzania ujumbe ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb).
Akizungumza
katika kikao hicho, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi
Chana (Mb) amewakaribisha wataalamu saba kutoka nchini Cuba waliowasili nchini
kwa ajili ya kufanya tafiti ya kina kuhusu changamoto ya mimea vamizi
inayozikabili hifadhi mbalimbali za taifa na maeneo mengine yaliyohifadhiwa
lengo ikiwa ni kutafuta ufumbuzi wa uhakika katika kukabiliana na changamoto
hizo.
“Napenda
kutambua kwamba, mimea vamizi ni tishio kubwa la uhifadhi nchini Tanzania, hasa
katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Ngorongoro na Bonde la Ziwa
Victoria. Spishi hizi, asilia na ngeni, zimevuruga mifumo ikolojia, mimea
asilia iliyohamishwa, na kuathiri vibaya makazi ya wanyamapori, utalii, ardhi
ya malisho na jamii za wenyeji. Spishi hizi vamizi zimeharibu mazingira na
kuathiri utalii,” amesisitiza Mhe. Chana.
Amefafanua
kuwa uwepo wa mimea vamizi ulisababishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli
za kibinadamu, kama vile kilimo, biashara ya mimea ya mapambo, na mipango ya
kudhibiti mmomonyoko wa udongo.
Kupitia
wataalam hao kutoka Cuba, Tanzania itapata utaalamu wa teknolojia bora ya
kukabiliana na mimea vamizi na kuendeleza uhifadhi nchini.
Kikao hicho
kimehudhuriwa na baadhi ya Watendaji kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Maliasili na Utalii na Utalii.
0 Maoni