Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa leo Februari 18, 2025 amefanya
mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Christine Grau, Ofisini
ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
Tanzania itaendelea kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji
na nchi za Umoja wa Ulaya.
“Inatia faraja sana kuona kuna ukuaji wa biashara na
uwekezaji kati ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya, Umoja wa Ulaya umewekeza
takriban euro bilioni tatu nchini, hii kwa kiasi kikubwa imechangia kutengeneza
ajira na makusanyo ya kodi. ”
Amesema kuwa Tanzania itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya
uwekezaji ili kuzivutia sekta binafsi kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Tanzania
inathamini msaada mkubwa ambao unatolewa na Umoja wa Ulaya katika kuchangia
shughuli za maendeleo nchini.
“Katika kipindi cha
2021-2027, Umoja wa Ulaya umetenga euro milioni 703 ili kusaidia mipango
mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania, tunakushukuru hasa kwa kujitolea kwenu
kuimarisha ushirikiano huu. ”
Awali, Mheshimiwa Majaliwa alikutana na Balozi wa Jamhuri ya
Korea, Ahn-Eun-Ju ambaye alimweleza kuwa Tanzania inajivunia ushirikiano na
nchi hiyo kwenye sekta mbalimbali za maendeleo.
“Tanzania na Jamhuri ya Korea zinaushirikiano mkubwa wa
kibiashara kwa miaka mingi, mnamo mwaka 2023, kiwango cha ufanyajibiashara
kilifikia dola milioni 672.7, ikilinganishwa na dola milioni 280.4 mwaka 2022.”
“Tunatambua kuwa
makampuni ya Jamhuri ya Korea yamewekeza katika sekta mbalimbali nchini
Tanzania, kama vile viwanda, usafirishaji na ujenzi, hivyo kuchangia maendeleo
ya nchi zetu. Tunathamini uwekezaji huu. ”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa alimweleza balozi huyo kuwa aone
namna ya kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata nafasi za kazi nchini Korea
hasa kwenye sekta ya uzalishaji. “Kwa upande wetu sisi tutahakikisha Watanzania
wanakuwa na vigezo stahiki vinavyohitajika ili waweze kufanya kazi. ”
Kwa upande wake Balozi Ju alimweleza Mheshimiwa Majaliwa kuwa katika kipindi chote atakachohudumu kama balozi nchini atahakikisha anasimamia na kuendeleza masuala ya uwekezaji kwa faida ya nchi zote mbili.
0 Maoni