Jumla ya
taasisi 551 zimeanza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuachana na
matumizi ya kuni na mkaa ikiwa ni katika jitihada za kuunga mkono Serikali
kupunguza ukataji miti na kulinda afya za wananchi.
Hatua hiyo,
ni katika utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za Umma
na Binafsi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya mia moja.
Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis
amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Februari 12, 2025 wakati akijibu swali
la Mbunge wa Rungwe Mhe. Anton Mwantona aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango
gani wa kuhakikisha taasisi zinazohudumia watu wengi zinaweka mifumo ya majiko
ya gesi ili kuokoa mazingira.
Akiendelea
kujibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali tayari imesaini
makubaliano ya awali na wawekezaji mbalimbali ikiwemo makampuni ya Oryx, Taifa
Gas, Lake Gas na Manji’s gas kuhusu kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 8.64
kwenye nishati safi ya kupikia.
Mhe. Khamis
amefafanua kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza mzigo wa gharama kwa watumiaji
wa nishati safi ambapo jumla ya majiko 452,455 yamepata ruzuku.
Aidha,
amesema Serikali inaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanzisha Mfuko wa
Nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato
cha chini kumudu bei ya gesi.
Hivyo, Mhe.
Khamis amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha uandaaji
wa Kanuni ya Katazo la Matumizi ya Kuni na Mkaa kwa Taasisi zinazolisha watu
zaidi ya 100 kwa siku zitakazojumuisha taasisi za umma na binafsi.
Akijibu swali
la nyongeza la Mhe. Mwantona aliyetaka kufahamu kama Serikali iko tayari kutoa
ruzuku kwa wawekezaji wakubwa ili taasisi zenye watu zaidi ya 100 zikawekewa
majiko ya gesi, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali imeweka mpango madhubuti
wa kutekeleza mkakati wa kuhakikisha jamii inahamia katika matumizi ya nishati
safi ya kupikia.
Amesema kuwa
ili kufanikisha hatua hiyo, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha
Mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia (Cook Fund) utakaowezesha taasisi, vikundi na
watu binafsi kuwezeshwa ili kupata majiko pamoja na kuwekewa miundombinu ya
nishati safi ya kupikia.
Pamoja na
hatua hiyo ameongeza kuwa tayari Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
kwa miaka 10 (2024-2034) ambao unatoa mwongozo wa utoaji wa elimu kuhusu
umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia umezinduliwa.

0 Maoni