Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewakaribisha wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.
Akizungumza
leo Februari 12, 2025 jijini New Delhi,
India katika Mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka India, Sudan, Malawi,
Rwanda, Nepal, Brazili pamoja na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali kutoka India
Dkt. Biteko amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha Nishati Safi ya Kupikia inapatikana kwa
urahisi na gharama nafuu.
Mwaka 2022
Serikali ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan ilisisitiza matumizi ya nishati safi na kueleza athari za
matumizi ya nishati isiyokuwa safi kwa kuanzisha mjadala wa kwanza kuhusu
matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na faida zake kiuchimi na Kijamii.
Dkt.
Biteko ametaja fursa mbalimbali za
biashara ya Nishati Safi ya Kupikia nchini Tanzania, kama vile ujenzi wa miundombinu
ya uzalishaji, kupokea, kuhifadhi na kusambaza nishati safi ya kupikia.
Fursa zingine
ni vituo vya kupokea LPG, vifaa vya uhifadhi, miundombinu ya usambazaji wa gesi
asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na maeneo jirani,
usambazaji wa LNG wa kiwango kidogo, vifaa na mitungi ya gesi asilia.
“ Ningependa
kuchukua fursa hii kuwataka wadau wote na wawekezaji katika sekta ya nishati
kujiunga nasi katika malengo yetu makubwa lakini yanayoweza kufikiwa ya kupata
umeme na nishati safi ya kupikia kuongeza sehemu ya nishati mbadala katika
mchanganyiko wa nishati na kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi ili kusaidia
upatikaji wa nishati,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja
jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia “Tanzania
imekamilisha maendeleo ya Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa
mwaka 2024-2034 wenye lengo kuu la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania
wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.”
Ameongeza
kuwa uzoefu unaonesha kuwa “ Katika kujifunza India imefanya vizuri katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na
takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2023,
asilimia 71.1 ya watu wa India walikuwa wakitumia nishati safi ya kupikia. Hii
imetokana na umuhimu wa kuhusisha sekta binafsi na kuunganishwa kwa ruzuku kwa
kaya zenye kipato cha chini,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko
amesema takriban watu bilioni 2.3 duniani hawapati nishati safi ya kupikia na
watu milioni 990 Kusini mwa Jangwa la Sahara hawajafikiwa matumizi na nishati
safi. “Hali hii inasababisha matatizo ya afya, uharibufu wa mazingira na
matatizo ya kiuchumi.”
Vilevile,
amesema Rais Samia amedhamiria kuinadi ajenda ya nishati safi ya kupikia nje ya
mipaka ya Tanzania na Afrika, ambapo katika mkutano wa COP 28, alizindua Programu
ya Uwezeshaji wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Wanawake wa Afrika (AWCCSP),
iliyoelekezwa kukabiliana na changamoto kubwa za kijinsia, mazingira, afya, na
kiuchumi zinazowakabili wanawake na wasichana barani humo.
Akiendelea
kuelezea msimamo wa Tanzania katika kuhamasisha Ajenda ya Matumizi ya Nishati
Safi kimataifa, Dkt Biteko amesema mwaka 2024 Rais Samia alishiriki katika
Mkutano wa Juu wa Nishati Safi ya
Kupikia nchini Ufaransa ambapo alikuwa
Mwenyekiti mwenza, na takriban dola bilioni 2.2 ziliahidiwa kwa ajili kusaidia ajenda hiyo barani Afrika.
Aidha,
Tanzania kwa kushirikiana na Tume ya Nishati ya Afrika (AFREC) ilifanya Mkutano
wa Kiwango cha Juu kuhusu Kupikia Safi barani Afrika katika Mkutano Mkuu wa
Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 2024 pamoja na kuwa mwenyeji wa Mkutano wa
Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliyofanyika jijini Dar es salaam Februari 27
na 28 mwaka huu kwa ajili ya kueleza dhamira zao kuhusu Mikataba ya Nishati ya
Kitaifa.
Kwa upande
wake, Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Mhe. Hardeep Singh ametaja
madhara ya matumizi ya nishati isiyosafi
“Kumekuwepo na idadi ya vifo takribani milioni 2, lakini wanawake na
watoto wanapata madhara zaidi, huku wanawake wakitumia hadi saa 5 kila siku kwa
ajili ya kutafuta kuni na kuandaa chakula.”
Akielezea
mafanikio ya matumizi ya nishati safi nchini India, amesema sasa watu milioni
330 wameunganishwa na matumizi ya gesi au nishati safi.
“Nishati safi
sasa inapatikana kwa watu na maisha yamekuwa rahisi na shughuli zimeendelea kufanyika
kwa ufanisi, sioni kwa nini hatuwezi kufanya hivi kwa kila mwananchi inawezekana,” Amemalizia Mhe. Signh.
Kimsingi
mkutano huo wa Mawaziri wa Nishati unatajwa kuwa muhimu katika jitihada za
kuendeleza matumizi ya nishati safi duniani ambao umetoa fursa kwa mawaziri
waliohudhuria kueleza jitihada zinazofanyika za kukuza matumizi ya nishati safi
katika nchi zao.
Aidha, masuala ya sera, mila za watu, uhamasishaji, ubunifu, miundombinu ya usambazaji na wawekezaji yanatajwa kuwa mchango muhimu ya mafanikio ya matumizi ya nishati safi.

Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


0 Maoni