Waziri wa
Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa, Serikali ya Tanzania inatambua kuwa
ili kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR)
kifanye kazi kwa ufanisi, kinahitaji upatikanaji wa dhahabu ya kutosha (feed
stock) na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuweka mikakati
ya kufanikisha jambo hilo.
Aliyasema
hayo jana Februari 11, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza katika semina
iliyoandaliwa kwa ajili ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Mhe. Mavunde
alibainisha kuwa Serikali imeshafanya kikao cha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) na wadau wote muhimu ili kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji wa mitaji kwa
Watanzania kupitia mpango wa Export Credit Guarantee Scheme.
Aidha, Waziri
Mavunde alisema kuwa, Serikali
inaendelea na juhudi za kuhamasisha wachimbaji wadogo kuanza kuuza dhahabu yao
katika viwanda vya ndani ikiwemo GGR, jambo ambalo litawanufaisha kwa kupata
bei nzuri, kupunguza gharama za usafirishaji, na kufurahia punguzo la tozo
zilizowekwa kwa dhahabu inayosafishwa ndani ya nchi.
Dhamira ya Serikali katika Uongezaji
Thamani wa Madini
Mhe. Mavunde
alieleza kuwa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa madini yanayochimbwa
hapa nchini yanaongezewa thamani hapahapa nchini, hatua inayolenga kuongeza
mapato ya Serikali, kutoa ajira kwa Watanzania, na kusaidia sekta nyingine
zinazohusiana na madini, kama vile benki na viwanda vya vifaa vya uchimbaji
kuendelea kupata masoko.
Alisisitiza
kuwa, GGR ni kiwanda cha kisasa chenye hadhi ya kimataifa ambacho kimekuwa
chachu ya mabadiliko katika sekta ya madini nchini. “Tuna furaha kuona kwamba
sasa Tanzania inayo miundombinu ya hali ya juu kwa ajili ya usafishaji wa
dhahabu, jambo ambalo linaipa nchi yetu hadhi kubwa katika soko la madini
duniani,” amesema Mavunde.
Serikali yajivunia uwepo wa GGR
Waziri
Mavunde alieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge kuwa, Serikali ya Tanzania
inajivunia uwepo wa viwanda vya uongezaji thamani madini hapa nchini, ikiwa ni
sehemu ya mkakati wa kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania
kwa kiwango cha juu zaidi na kwamba mojawapo ya mafanikio makubwa katika Sekta
ya Madini ni uwepo wa Kiwanda cha kisasa cha kusafisha madini ya dhahabu, Geita
Gold Refinery (GGR), kilichopo mkoani Geita.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa alisisitiza kuwa, licha ya
dhamira njema ya Serikali kulinda viwanda vya ndani vya uongezaji thamani
madini, ipo haja ya vitengo vya masoko vya viwanda husika kufanya utafiti
kuhusu mbinu zingine za kimasoko kutokana na ushindani wa kibiashara ili kupata
malighafi nyingi zaidi bila kuvunja maadili yanayotakiwa kwa kuzingatia kuwa
viwanda hivyo vina hadhi ya kimataifa.
Mazingira Rafiki ya Kibiashara kwa
Wachimbaji wa Dhahabu
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba alifafanua kuwa, ili kusaidia upatikanaji wa kutosha wa Malighafi (Feed Stock) kwa GGR, Serikali imeweka mazingira bora ya kibiashara kwa wachimbaji wa dhahabu, ikiwa ni pamoja na kupunguza jumla ya tozo kwa dhahabu inayosafishwa katika viwanda vya ndani ikiwemo GGR, tozo zimepungua hadi asilimia 6.3, ikilinganishwa na asilimia 9.3 zinazotozwa katika masoko mengine.
Mhandisi
Samamba aliongeza kuwa, hatua hiyo imelenga kuwahamasisha wachimbaji wadogo na
wa kati kuuza dhahabu yao katika viwanda vya ndani kama GGR badala ya kuuza
katika masoko mengine ikiwa bado haijasafishwa kwa kiwango cha kimataifa.
Bunge Lapongeza Uwekezaji wa GGR
Naye,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. Mathayo David
kwa niaba ya kamati hiyo, alimpongeza Bi. Mwanahamisi Masasi, maarufu kama Mama
Masasi mmoja wa wawekezaji wakubwa katika mradi wa Geita Gold Refinery, kwa
uthubutu na hatua kubwa alizopiga katika kuanzisha na kuendeleza kiwanda hicho.
Dkt. Mathayo
alieleza kuwa, uwekezaji huo ni wa kihistoria na una manufaa makubwa kwa uchumi
wa nchi, hususan katika sekta ya madini huku akiitaka Serikali kupitia Wizara
ya Madini kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa aina hiyo katika madini mengine
pia ili kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika zaidi na
rasilimali zake za madini.



0 Maoni